UJUMBE wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) umeridhishwa na juhudi
zinazofanywa na Serikali ya Rais John Magufuli katika kuongeza juhudi za
kupambana na rushwa. Hali hiyo itabadili mtazamo wa awali kwamba
utawala bora ulishapotea nchini, kama ilivyoonekana katika tafiti nyingi
zilizofanyika.
Aidha, ujumbe huo unaunga mkono malengo ya uchumi yaliyomo katika
mwongozo wa Bajeti ya mwaka 2016/2017 uliochapishwa, ambayo yamezingatia
uhalisia katika ukadiriaji wa mapato.
Hayo yalielezwa katika taarifa ya shirika hilo, iliyotolewa kwa
vyombo vya habari jana Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa ziara ya
ujumbe huo ulioongozwa na Mkurugenzi Msaidizi na Mkuu wa IMF nchini,
Herve Joly. Ujumbe huo pia ulifanya tathmini ya nne ya Mpango wa Ushauri
wa Sera za Uchumi (PSI), ulioidhinishwa na Bodi Tendaji ya IMF mwaka
huu.
Ilieleza taarifa hiyo kuwa “ujumbe umeridhishwa na juhudi
zinazofanywa na serikali katika kuongeza juhudi zaidi za kupambana na
rushwa, hali ambayo itabadili mtizamo wa awali kwamba utawala bora
ulikwishapotea nchini kama ilivyoonekana kwenye tafiti nyingi
zilizofanyika.”
Tangu aingie madarakani Novemba mwaka jana, Rais John Magufuli na
serikali yake imejipambanua kwa kupambana na rushwa na ufisadi kwa
kuwachukulia hatua wakwepa kodi na watendaji wa serikali ambao ni wala
rushwa, kuwapeleka mahakamani na kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwongozo wa bajeti ya Tanzania kwa mwaka
2016/17 umezingatia kupunguza kwa kiasi kikubwa nakisi ya bajeti na
matumizi ya kawaida ili kutoa fursa ya kuongeza matumizi ya maendeleo.
“Changamoto kubwa katika kukamilisha bajeti ni kuhakikisha kuwa matumizi
yanaendana na mapato halisi. Majadiliano yataendelea katika wiki chache
zijazo ili kufikia muafaka juu ya mfumo mzima wa sera za uchumi ambazo
zitapelekwa kukamilisha mapitio ya nne ya mpango wa PSI,” ilieleza
taarifa hiyo.
Mapitio hayo ya mpango wa PSI na majadiliano chini ya kanuni ya nne
ya mkataba ulioanzisha IMF, yanatarajiwa kujadiliwa na Bodi Tendaji ya
IMF mwaka huu. Majadiliano chini ya mpango wa PSI pia yamelenga kwenye
utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 na mipango ya bajeti ya mwaka
2016/2017.
Post A Comment: