MSHAMBULIAJI mahiri wa Yanga raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma, amesema
amejipanga kuhakikisha anaifikisha timu yake kwenye hatua ya makundi ya
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.
Ngoma amejiunga na Yanga msimu huu akitokea FC Platinum ya Zimbabwe
na tayari ameonesha uwezo mkubwa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara na
kuisaidia timu yake kuwa katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.
Mshambuliaji huyo aliyeifungia Yanga mabao 13 kwenye Ligi Kuu
Tanzania Bara msimu huu, alisema sababu ya kutoa kauli hiyo ni kutokana
na kiwango chake kuwa juu na ushirikiano mzuri kutoka kwa wachezaji
wenzake waliopo kwenye kikosi cha kocha Mholanzi Hans Pluijm.
“Ni michuano migumu hasa hatua tuliyopo hivi sasa, lakini Yanga ni
timu kubwa, wachezaji lazima tuoneshe vipaji vyetu ili kuipa mafanikio
timu hii na hatimaye tuweze kufikia hatua ya makundi au hata tucheze
fainali mwaka huu,” alisema Ngoma.
Mzimbabwe huyo alisema amejipanga kuhakikisha Yanga ya msimu huu
inavunja rekodi kwa kuwatoa mabingwa wa zamani wa Afrika, Al Ahly kwenye
raundi ya pili ya michuano hiyo ya Afrika.
Alisema anajua hiyo ni timu kubwa Afrika, lakini haoni sababu ya
kuwahofia kwa sababu hata wao wana timu nzuri ambayo kama watacheza kwa
kujituma wanaweza kuwatupa nje ya michuano hiyo na kujiwekea rekodi ya
kuwatoa mabingwa hao wa zamani.
“Nimesikia kuwa mara nyingi Yanga imekuwa ikitolewa kwenye michuano
ya kimataifa na timu za kiarabu, nataka mwaka huu iwe tofauti kwa
kufanya maajabu ya kuwatoa Al Ahly, kwa sababu tuna timu nzuri ambayo
inaweza kufanya vizuri kama tutacheza kwa ushirikiano,” alisema Ngoma.
Mshambuliaji huyo amelitaka benchi la ufundi pamoja na wachezaji
wenzake kujiwekea mikakati maalumu kwa ajili ya mchezo huo ili waweze
kufanya vizuri na kufanikisha kile ambacho wamekikusudia.
Post A Comment: