Chama cha soka nchini Uholanzi KNVB huenda kikamtangaza meneja wa
klabu ya Man Utd, Louis van Gaal kuwa mkurugenzi wa ufundi, endapo
atasitishiwa mkataba wake na uongozi wa Man Utd mwishoni mwa msimu huu.
Van Gaal, amekua katika minong’ono ya kutimuliwa kazi mwishoni mwa
msimu huu, na nafasi yake kuchukuliwa na meneja kutoka nchini Ureno Jose
Mourinho, kutokana na matokeo ya kikosi cha Man Utd kutokua mazuri kwa
msimu wa pili tangu alipoanza kazi mwaka 2014.
Kamati ya utendaji ya chama cha soka nchini Uholanzi, inaamini Van
Gaal anafaa kuwa mkuu wa ufundi katika soka la nchini humo, kutokana na
uzoefu alioupata tangu alipoanza shughuli za ukufunzi mwaka 1986 akiwa
kama meneja msaidizi wa klabu ya AZ Alkamar.
Kushindwa kufuzu katika fainali za mataifa ya bara la Ulaya za mwaka
2016 (Euro 2016) kumewafanya viongozi wa KNVB kuamini kuna mahala
walipokosea, na hakuna dawa ya kurekebisha kosa hilo zaidi ya kumrejesha
Van Gaal ambaye alikuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uholanzi wakati
wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014.
Viongozi wa KNVB, wanaamini mipango na mikakati iliyotumiwa na Van
Gaal wakati anasaka nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka
2014, ataitumia akiwa kama mkurugenzi wa ufundi kwa kusaidina na kocha
mkuu wa timu ya taifa.
Van Gaal mwenye umri wa miaka 64, alifanikiwa kukiongoa kikosi cha
Uholanzi katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, kule nchini
Brazil na kumaliza kwenye nafasi ya tatu baada ya kuwafunga wenyeji
mabao matatu kwa sifuri.
Post A Comment: