MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela amewataka wakazi wa
kata ya Mwakata, wilayani Kahama ambao waliahidiwa kujengewa nyumba na
serikali baada ya kuathiriwa na mvua ya mawe kuvuta subira wakati
serikali iliyopo madarakani ikitekeleza ahadi iliyotolewa.
Serikali ya awamu ya nne iliahidi kujenga nyumba 342 za walioathirika
na mvua ya mawe iliyosababisha zaidi ya watu 48 kupoteza maisha.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Mwakata siku tatu baada ya kuripoti
katika kituo kipya cha kazi, Kilango alisema kuwa ucheleweshwaji wa
ujenzi ulitokana na Serikali kuelekeza nguvu kufanikisha uchaguzi mkuu
uliopita.
Mkuu huyo Mpya wa Mkoa wa Shinyanga alisema kuwa kutokana na uchaguzi
huo kuisha kwa sasa Serikali itahakikisha kuwa hakuna mkazi yeyote wa
kata ya Mwakata atakayeendelea kuishi kwa jirani.
“Kwa sasa uchaguzi umepita na tuiachie Serikali ifanye kazi yake ya
ujenzi wa nyumba hizo na mimi ninawaahidi kuwa nitasimamia ujenzi huo,
kwani maafa kama haya yalishawahi kutokea katika jimbo langu za Same
enzi za ubunge wangu na Serikali ilichukua muda wa miaka miwili kutatua
tatizo kama hilo”, alisema Kilango.
Post A Comment: