MSHAMBULIAJI mpya wa timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’,
Abdillahie Yussuf, amefurahi kuitwa kuichezea nchi yake na kuahidi
kufanya maajabu.
Abdillahie ambaye pia anajulikana kama Adi, anacheza Mansfield
inayoshiriki Ligi Daraja la Pili England, amesema amefurahi kuona
anaungana na wachezaji wengine kuitumikia nchi yake na kuahidi kutoa
ushirikiano.
“Nafurahi kuichezea nchi yangu, hivyo sitawaangusha Watanzania,
endapo nitapata nafasi ya kucheza ila joto linanipa shida kidogo, lakini
nitazoea,” alisema.
Alisema amezaliwa Tanzania na baadae wazazi wake walihamia Uingereza,
ambako ndiko alikokulia, pia amefurahi kukutana na Mbwana Samatta
mchezaji ambaye ameing’arisha Tanzania baada ya kuwa mchezaji bora wa
Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika.
Naye Mshauri wa Benchi la Ufundi la Taifa Stars, Abdallah Kibadeni
amesifu kiwango cha mshambuliaji huyo na kudai ataisaidia timu.
“Kwa muda mchache niliomwona nimeridhika na kiwango chake na naamini
ataweza kuisaidia timu na nchi kwa ujumla,” alisema Kibadeni.
Adi ambaye anacheza namba tisa, alizaliwa Februari 20, 1992 na
alianza kucheza soka akiwa kwenye Akademi ya Leicester City 2008-2011,
2011-2013 alicheza Burton Albion, 2013-2014 alikuwa Lincolin City na
2014 -2015 Oxford City.
Post A Comment: