Msanii wa nyimbo za injili nchini, Rose Mhando, ameshtakiwa kwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, kwa
kitendo cha utapeli na kushindwa kutekeleza mkataba wa kuhudhuria na
kutumbuiza kwenye Tamasha la Pasaka lililofanyika jijini Mwanza licha ya
kulipwa gharama zote alizotaka.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions inayoongozwa na Alex Msama,
ambayo ina mkataba naye imekuwa ikiuza na kuandaa matamasha ya msanii
huyo pamoja na tamasha la Pasaka la kila mwaka, alimweleza Waziri
Nnauye, mbele ya halaiki ya wananchi alipokuwa mgeni rasmi wa sherehe za
tamasha hilo lililofanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza na mikoa ya
Kanda ya Ziwa.
Msama alieleza kusikitishwa na kitendo cha Rose Mhando kuingia mitini
ilihali akiwa ameingia mkataba na kulipwa gharama zote pamoja na nauli
alizodai kabla ya kuanza safari kufika Geita, Mwanza na Kahama kujiunga
na wasanii wenzake kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha hilo.
“Mheshimiwa Waziri, Rose Mhando naye amekuwa ni jipu kwa kuwa
amefanya utapeli kwa kukubali kulipwa gharama zake zote lakini
ameshindwa kuhudhuria na kutumbuiza kama wenzake wakina Solomon Mkubwa,
Bonny Mwaitege, Upendo Nkone na wengine uliowashuhudia hapa.
“Hii ni mara ya tatu amekuwa akifanya hivi na mara kwa mara nimekuwa
nikimsamehe,” alisema bila kutaja kiasi alichomlipa katika mkataba
waliokubaliana ili aweze kufanya onyesho hilo.
Msama pia akatumia fursa hiyo kuwaomba radhi wananchi waliofika
katika Uwanja wa CCM Kirumba kwa kutegemea mwimbaji huyo angekuwepo na
kutumbuiza na wenzake lakini kilichotokea ni aibu na utapeli wa msanii
huyo mkubwa wa nyimbo za injili aliyejizolea umaarufu ndani na nje ya
nchi.
“Kuanzia leo mtu yeyote asije akaingizwa mjini na Rose Mhando kwa
kuingia naye makubaliano akidhani yupo chini ya Kampuni ya Msama
Promotions, kwa kitendo alichoendelea kukifanya naomba kutangaza rasmi
kuvunja mkataba wa kufanya kazi na msanii huyo ili kulinda hadhi na
heshima ya Kampuni yangu,” alisisitiza Msama.
Post A Comment: