WAKUU wa mikoa 26 ya Tanzania Bara wamekabidhi ripoti za uhakiki wa
watumishi hewa katika mikoa yao, ambazo zimeonesha kuwa na watumishi
hewa zaidi ya 2,000, huku Mkoa wa Shinyanga ukiwa hauna mtumishi hewa
yeyote wakati Mwanza ndio kinara ukiwa na watumishi hewa 334.
Watumishi hao zaidi ya 2,000 wameisababishia serikali hasara zaidi ya
Sh bilioni nne, huku mikoa ya Mwanza, Singida, Kigoma, Pwani, Dodoma,
Morogoro na Kilimanjaro ikionekana kuwa na idadi kubwa ya watumishi
hewa.
Ripoti hizo ziliwasilishwa jijini Dar es Salaam jana na Wakuu wa
Mikoa hao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ambaye alisema ripoti hizo
atazifikisha kwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi kwa ajili ya
kuhakikiwa, kabla ya kuwasilisha kwa Rais John Magufuli.
“Nitazipeleka kwa Waziri wa Utumishi ili yeye azifanyie uhakiki na
zipitiwe upya…hata kwenye wizara pia ufanywe uhakiki wa watumishi hewa
kwa sababu unaweza ukakuta hata wizarani wapo. Hili suala nitalifikisha
kwa Waziri wa Utumishi,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa baada ya
kukamilika itafikishwa mbele ya Rais Magufuli.
Aidha, aliwataka wakuu hao wa mikoa, kutambua mamlaka yao na
kuyatumia ipasavyo ili kila aliyehusika kwa namna moja au nyingine
katika watumishi hao hewa anachukuliwa hatua haraka ipasavyo. Awali,
wakiwasilisha ripoti zao, baadhi ya wakuu wa mikoa walisema kuwa bado
hawajapata idadi kamili ya fedha zilizopotea kutokana na idadi ya
watumishi hewa katika mikoa yao.
Akiwasilisha ripoti yake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda
alisema wamebaini kuwepo kwa watumishi hewa 270 ambao wamesababisha
hasara ya Sh bilioni 1.8 katika kipindi cha mwaka mmoja. Wengine
waliowasilisha na idadi ya watumishi hewa kwenye mabano ni Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza, John Mongella (334). Alisema bado hawajapata idadi halisi ya
hasara kutokana na watumishi hao kulipwa mishahara.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigume aliwasilisha (231) na
hawajapata gharama halisi za fedha walizochota. Mikoa mingine
iliyowasilisha ripoti na idadi ya watumishi hewa kwenye mabano ni Kigoma
(171) hasara Sh milioni 104.6, Pwani (150) hasara bado haijapatikana,
Dodoma (139) hasara ni Sh milioni 287 kwa kipindi cha miezi sita,
Morogoro (122) hasara ni zaidi ya Sh milioni 450, Kilimanjaro (111)
hasara Sh milioni 281.4.
Mingine ni Tanga (104) hasara bado haijapatikana, Mbeya na Songwe
(98) hasara ni Sh milioni 459.6, Mara (94) hasara Sh milioni 121, Dar es
Salaam (73) hasara Sh milioni 316, Lindi (57) hasara Sh milioni 36.2,
Tabora (38) hasara Sh milioni 118.7 na Ruvuma (37) hasara Sh milioni 58.
Mkoa wa Simiyu (62) hasara Sh milioni 320, Njombe (34) hasara Sh
milioni 20.1, Katavi (21) hasara Sh milioni 20.7, Manyara (50) hasara Sh
milioni 42, Iringa (15) hasara haijapatikana na Kagera (14) hasara Sh
milioni 49.1.
Akitoa siri ya mkoa wake kutokuwa na watumishi hewa, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Anne Kilango Malecela alisema viongozi waliotangulia kabla
yake, waliweka mikakati mizuri jambo lililowezesha wasiwepo watumishi
hao. “Viongozi waliokuwepo walianza zoezi hili tangu mwezi Julai mwaka
jana na kila tarehe 26 ya mwisho wa mwezi walikuwa wakihakiki watumishi
wao hivyo ndio maana hakuna watumishi hewa,” alisema Anne- Kilango,
ambaye katika Serikali ya Awamu ya Nne alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema katika mkoa wake yapo
majina ya watumishi hewa, ambayo yapo katika orodha ya malipo ya
mishahara, na kutoa mfano wa Manispaa ya Tabora peke yake hasara
iliyotokana na kulipa watumishi hewa ni Sh milioni 24. Machi 15, mwaka
huu wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa, Rais Magufuli alitoa siku 15 kwa
viongozi hao kuhakikisha wanajumuisha wafanyakazi wote na kuwaondoa
watumishi hewa.
Aidha, juzi Rais Magufuli alisema uhakiki mdogo uliofanywa hivi
karibuni kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa nchini, umebaini wafanyakazi
hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa Sh bilioni 1.8. Alisema ni matarajio kuwa
uhakiki unaofanywa nchi nzima, utaisaidia serikali kubaini wafanyakazi
hewa wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za Watanzania.
Post A Comment: