WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ameuagiza Wakala wa
Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kusitisha mara moja usajili mpya wa
wadhamini wa asasi, vyama, misikiti na vikundi mbalimbali vya kijamii
kwa lengo la kufanya uhakiki wa uhalali wa kuwepo wa taasisi hizo
kisheria.
Ameagiza kuwa uhakiki huo ukamilike ndani ya miezi mitatu (siku 90)
kuanzia sasa na orodha kamili ya wadhamini ikiwa ni pamoja na picha zao,
anuani ya posta na makazi, na taarifa nyingine muhimu za utambuzi wa
taasisi hizo mahali zilipo. Taarifa hizo ziwasilishwe Rita na nakala
wizarani kwa uhakiki na kumbukumbu.
Dk Mwakyembe alitoa agizo hilo, alipokutana na watendaji na uongozi
wa Bodi ya Rita, Dar es Salaam jana kwa lengo la kuboresha utendaji wa
Wakala na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano. Rita ina zaidi
ya wadhamini 5,000 walio kwenye vitabu vyao vya usajili.
Aidha, Waziri huyo ameitisha kikao wiki ijayo cha mamlaka zote
zinazohusika na usajili wa vikundi vya kijamii, mashirika, kampuni na
asasi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha taratibu za usajili na
uendeshaji na kuboresha mawasiliano baina ya vyombo vya usajili vya dola
ili kulinda maslahi mapana ya Taifa.
Post A Comment: