KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imewaweka kitimoto mawaziri, Gavana wa Benki Kuu (BoT) na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kutokana na kutoridhishwa na hali ndani ya mifuko ya jamii.
Katika kikao hicho kilichokuwa chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Richard Ndassa, wabunge walieleza kusikitishwa na hali ilivyo ndani ya
Mfuko wa Pensheni wa PSPF hatua inayotishia uhai wake, na pia kutolipwa
kwa deni analodaiwa mfanyabiashara Yusuf Manji na PSPF.
Wabunge pia walieleza kushangazwa na hatua ya SSRA kuendelea kukaa
kimya huku kukiwa na madai kwamba kuna ubadhirifu wa mabilioni ya fedha
na uwekezaji mbovu ndani ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mawaziri walioitwa mbele ya kamati hiyo ni Waziri wa Fedha na Mipango
aliyewakilishwa na Naibu Waziri Dk Ashatu Kijaji, Waziri wa Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu ambaye aliwakilishwa na Naibu Waziri
Antony Mavunde na SSRA iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Irene Isaka.
Akizungumza na watendaji hao wa Serikali, Mwenyekiti Ndassa ambaye ni
Mbunge wa Sumve (CCM), alisema kuitwa kwao kwa Kamati hiyo kunatokana
na jukumu iliyokabidhiwa na Bunge la kusimamia uwekezaji na mitaji ya
umma ili kuhakikisha mashirika ya umma yanafanya uwekezaji mzuri na
wenye tija.
Kuhusu Mfuko wa Hifadhi wa PSPF, Ndassa na wabunge wote waliochangia,
walisema Mfuko huo upo katika hatari ya kufa, kutokana na kukabiliwa na
nakisi kubwa ya kifedha hatua inayofanya ushindwe kulipa mafao ya
wastaafu wa serikali hususan walimu kwa muda mrefu sasa.
“Tumewaita kutokana na hatari ya Mfuko wa PSPF kufa. Kama Mfuko huu
utakufa, watakaopata shida ni wastaafu na hasa walimu. Majimboni nchini
kote hakukaliki. Wastaafu wanawasumbua wabunge maana hawalipwi mafao yao
wakati wao walitoa fedha zao,” alisema Ndassa.
Post A Comment: