Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi
Maalum wa Umoja wa Afrika wa Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya, amewasili
jana Jijini Tunis nchini Tunisia kushiriki Mkutano wa 8 wa Nchi
majirani wa Libya.
Mkutano huo umeitishwa na Serikali ya Tunisia, na ni muendelezo wa
jitihada za nchi majirani kusaidia kuleta hali ya amani na usalama
nchini Libya.
Rais Mstaafu Kikwete amewasili Tunis akitokea Salalah nchini Oman
alikoshiriki Mkutano wa Kamati ya Bunge la Kuandika Katiba ya Libya.
Akiwa Jijini Tunis, Jana tarehe 22 Machi, 2016 Dkt. Kikwete amefanya
mazungumzo na Waziri wa Masuala ya Maghreb, nchi za Kiarabu na Afrika,
wa Algeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh, aliyemtembelea hotelini
kwake.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Messaleh amempongeza Rais Mstaafu
Kikwete kwa kuteuliwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kusuluhisha
mgogoro wa Libya. Amemueleza hali ya usalama na kisiasa ya Libya na
mtizamo wa nchi yake juu ya namna bora ya utatuzi wa mgogoro huo, na
akamhakikishia ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika jukumu lake
alilokabidhiwa na Umoja wa Afrika.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu Kikwete amemshukuru Waziri Abdelkader
Messaleh kwa maelezo yake na ushirikiano aliomuahidi na akamueleza
matumaini yake ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo hasa ikizingatiwa
kuwa nchi jirani na Libya na Umoja wa Afrika zitashirikiana na wadau
wote kuhakikisha mgogoro huo unatatuliwa.
Rais Mstaafu Kikwete amesisitiza kuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa Libya liko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe.
Katika ziara yake nchini Tunisia, mbali na kuhudhuria Mkutano wa 8
wa nchi jirani na Libya, Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa pia kukutana
na Waziri Mkuu Mteule na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Libya,
(Presidency Council) Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj, wadau wengine wa
Libya pamoja na kutembelea Ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika kwa Libya
iliyoko jijini Tunis.
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 25 Machi, 2016
Post A Comment: