Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefika
nyumbani kwake katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita
kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais,
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika
uwanja wa shule ya sekondari Chato, ametoa wito kwa kila mtanzania
kuchapa kazi kwa juhudi ili nchi iondokane na utegemezi wa misaada ya
wafadhili ambayo huambatana na masharti.
Dkt. Magufuli amesema jukumu kubwa lililo mbele ya watanzania kwa
sasa, ni kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila mmoja
ahakikishe anaongeza uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.
"Kwa hiyo ni lazima tujisimamie sisi wenyewe, na tukijisimama sisi
wenyewe kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni mfanyakazi
afanye kazi kwelikweli, kama ni mkulima afanye ukulima wake kwelikweli,
kama ni mfanyabiashara afanye biashara kwelikweli, kama ni mfugaji afuge
kwelikweli, kama ni mvuvi avue kwelikweli, Tanzania hii tutavuka"
Amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesema serikali yake imeamua kuchukua hatua
kudhibiti nidhamu serikalini, kwa kuhakikisha inawachukulia hatua
watumishi wa umma wanaolisababishia taifa upotevu mkubwa wa fedha, na
ameahidi kuwa hatua hizo maarufu kwa jina la "Kutumbua Majipu"
zitaendelea kuchukuliwa hadi tatizo hilo likomeshwe.
Post A Comment: