KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imemwomba Rais
John Magufuli kuangalia tatizo la uhaba wa sukari nchini na kuona jinsi
ya kufanya kuruhusu kutoa vibali kwa wafanyabiashara kuagiza sukari nje
ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Dk Mary Nagu alisema uhaba wa sukari nchini kwa sasa ni
kati ya tani 80,000 hadi 100,000 na kwamba kama hatua za haraka
hazitachukuliwa, bidhaa hiyo itahadimika na wananchi watalanguliwa.
“Tumekutana na Bodi ya Sukari, na tumezungumza nao, wametuambia kuna
upungufu wa sukari ya matumizi ya nyumbani kati ya tani 80,000 hadi
100,000, tunamuomba Rais na serikali yake kuangalia jambo hili na kuona
umuhimu ya kuruhusu kiasi hicho cha sukari kiingizwe,” alisema Dk Nagu.
Alisema kabla ya nchi kubinafsisha viwanda vya sukari ilikuwa
inazalishwa kwa mwaka tani 100,000 na baada ya kubinafsishwa viwanda vya
ndani vinazalisha tani 320,000 ilhali mahitaji ni tani 420,000.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku uingizaji wa
sukari kutoka mataifa ya kigeni ili kuvilinda viwanda vya sukari nchini
humo ambavyo vimeathiriwa na uingizaji wa sukari ya bei rahisi kutoka
nje.
Post A Comment: