Ili uweze kufanikiwa vizuri
katika biashara yako, kwenye kipindi hiki chenye ushindani wa kila namna, unahitaji kuwa mipango imara na utaratibu
mzuri utakaoweza kufanya biashara yako ikasimama kwa muda mrefu bila
kuteteleka. Watu wengi huwa wana mawazo ya kufikiri kuwa wana uwezo wa
kutengeneza pesa na faida kubwa mara moja katika biashara zao kwa kuwa wana mtaji na uwezo wa kufungua
biashara wanao.
Kwa mawazo hayo, huwa yakiwapoteza
wengi kutokana na ukweli kwamba mambo mengi yamebadilika kwenye biashara kwa
sasa tofauti na siku za nyuma. Kitendo cha wewe kuwa na mtaji mkubwa siyo
kipimo cha mwisho cha kukuhakikishia ni lazima biashara yako itatoa faida kubwa
kama unavyofikiri. Yapo mabadiliko na mambo ya lazima ambayo unatakiwa uyafanye
ili kuweza kutengeneza pesa za kutosha na si mtaji pekee tu.
Wapo watu ambao walianza na
mitaji mikubwa katika biashara zao lakini hawakuweza kuona matokeo makubwa kama
walivyofikiri. Na pia wapo watu walianza na mitaji midogo waliweza kufanya
vizuri na kupata faida kubwa sana. Ninachotaka kukuonyesha hapa ni ujue kuwa yapo mambo ya ziada unayotakiwa uyajue
mbali na mataji ili ufanikiwe. Lakini,
sio nia yangu kukuonyesha uzuri ama ubaya wa mtaji mdogo au mkubwa katika
biashara yako.
Kwa kuweza kujua mambo hayo
itakusaidia hatua kwa hatua, kujenga biashara itakayoweza kukupa faida. Watu
wenye mafanikio makubwa kibiashara, moja
ya siri kubwa wanayoitumia katika biasha zao ni kufanyia kazi mambo hayo kila
siku. Hiki ndicho kitu tunachotaka ujue leo hapa kupitia makala hii. Ni mambo
gani yatakayoweza kukusaidia kutengeneza biashara itakayokupa faida kubwa na
endelevu?
Haya
Ndiyo Mambo 6 Ya Kukusaidia Kutengeneza Biashara Itakayokupa Faida Kubwa.
1.
Kuwa mbunifu.
Ipo nguvu kubwa sana ya
kimafanikio ikiwa utakuwa mbunifu katika biashara yako. Bila kuwa na ubunifu
wowote ule muhimu katika bishara yako, elewa utaachwa nyuma sana. Kwa kuwa
mbunifu itakusaidia kujua ni wapi ulipo na uboreshe biashara yako eneo lipi ili
uweze kushinda nguvu ya ushindani.
Kwa kadri unavyozidi kuwa
mbinifu ndivyo mafanikio makubwa yanazidi kuwa upande wako. Biashara yoyote ile
yenye mafanikio makubwa, ndani yake huwa ina ubunifu. Hili ni jambo mojawapo
muhimu sana litakalokuwezesha kukusaidia kutengeneza biashara itakayokupa faida
kubwa, ikiwa utalizingatia.
2.
Kuwa tayari kwa ushindani.
Hiki ndicho kitu ambacho
hutakiwi kukiogopa hasa linapokuja suala ushindani katika biashara. Kikubwa
unachotakiwa kujua hapa ni hao washindani wako wanafanya nini cha ziada tofauti
na wewe, ili nawe uweze kujifunza na ikiwezekana ufanye kama wao na pengine
kuzidi zaidi ya hapo walipo. Kwa kufanya hivyo itakusidia kukabiliana na
ushindani na kufikia malengo yako.
3.
Kuwa na utaratibu wa kuweka kumbukumbu.
Karibu wafanyabishara wote
wenye mafanikio makubwa huwa wana utaratibu wa kuweka kumbukumbu katika
biashara zao. Kwa kuweka kumbukumbu muhimu itakusaidia sana kujua ni wapi
ambapo unakumbana na changamoto na pia kujua ni eneo lipi unalopaswa
kuliboresha zaidi. Hii ndiyo siri mojawapo unayoweza kuitumia kutengeneza faida
katika biashara yako.
4.
Kuwa tayari kujitoa mhanga.
Katika kipindi ambacho ndio
kwanza biashara yako inaanza, ili kufanya biashara yako ikue kwa kasi
unalazimika kujitoa mhanga ama kuchua ‘Risk’.
Hii ndio njia muhimu itakayoweza kukuza biashara yako. Kuna wakati utalazimika
kufanya kazi zaidi kuweza kujifunza hata kwa wengine ili kuona matokeo
unayoyataka yawe kwako. Bila kujitoa mhanga juu ya biashara yako utachelewa
kufika kule unakotaka kufika.
5.
Kuwa mvumilivu.
Kuna wakati mambo yanaweza yakawa mabaya na yakakuendea
kinyume na ulivyotarajia, lakini kuwa mvumilivu. Hii ni nguzo muhimu kwako
ambayo unatakiwa kujishikilia bila kuachia mpaka ufanikiwe. Matatizo yoyote
yatakayo kupata kwenye biashara yako siyo mwisho wa mafanikio. Jifunze juu ya
changamoto hizo na kisha chukua hatua ya kuendelea mbele zaidi. Vinginevyo,
ukikata tamaa, utakuwa umejikwamisha wewe mwenyewe.
6.
Kuwa tayari kutoa huduma bora.
Hii naweza kusema ndio funga
kazi. Ukiweza kutoa huduma bora itakayoweza kukidhi matakwa ya mteja ujue
tayari umefanikiwa katika biashara yako. Nasema hivyo kwa sababu, suala la
kutoa huduma bora kwa wengi ni tatizo kubwa sana. Unaweza ukafanya uchunguzi
mdogo tu, utaelewa ukweli zaidi wa hili ninalosema. Acha kufanya biashara
ilimradi ufanye tu, jifunze kutoa huduma nzuri itakayomvuta mteja aje tena
kwako kesho.
CREDIT-dirayamafanikio.blogspot.com
Post A Comment: