MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange,
amemtumia salamu za pongezi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa tena na wananchi wa
Zanzibar kushika wadhifa huo kwa muhula wa pili cha madaraka.
Salamu hizo zilizotumwa na Jenerali Mwamunyange kwa niaba ya Maofisa,
Askari na Watumishi wa Umma wanaofanya kazi katika Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), zilieleza kuwa ushindi wa kishindo wa Dk
Shein alioupata unadhihirisha kuwa wananchi wa Zanzibar wameridhishwa na
uongozi wake makini na mahiri aliouonesha katika muhula wake wa kwanza
wa uongozi wake.
Salamu hizo ziliendelea kueleza kuwa historia ya Dk Shein ya
uaminifu, maadili mema na uzalendo aliouonesha katika utumishi wake wa
muda mrefu katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika kabla hajawa
Rais wa Zanzibar imewapa wananchi imani kubwa kuhusu uongozi wake.
“Mheshimiwa Rais, hapana shaka kuwa katika muhula huu wa pili wa
uongozi wako, Zanzibar itashuhudia mafanikio makubwa zaidi ya maendeleo
ya kiuchumi na kijamii, sambamba na kuendelea kuwepo kwa hali ya amani
na utulivu kwa wananchi wote,” ilieleza sehemu ya salamu hizo.
Aidha, salamu hizo za pongezi zilieleza kuwa JWTZ inamhakikishia Dk
Shein kuwa itaendelea na utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kwake kama
ilivyo desturi ya majeshi nchini. Wakati huo huo, Rais mstaafu wa Awamu
ya Pili Zanzibar, Abood Jumbe Mwinyi, naye amemtumia salamu za pongezi
Dk Shein kwa ushindi wa kishindo alioupata katika marudio ya uchaguzi wa
Zanzibar.
Post A Comment: