Mtoto Bahati Ally Kaminyoge mwenye umri wa miaka 12 amefanyiwa ukatili wa kutisha na wazazi wake baada ya kufungiwa ndani ya nyumba kwa zaidi ya miaka 10 bila kutoka nje,huku wakimnyima baadhi ya huduma muhimu za kibinadamu.
Taarifa za ukatili dhidi ya mtoto huyo zimetolewa na raia wema
ambao wamezifikisha kwa Mwenyekiti wa kituo cha haki za kibinadamu
mkoani Mbeya, Said Mohamed Madudu ambaye ameshirikiana na Ofisi ya
Maendeleo ya Jamii wilayani Mbozi pamoja na Jeshi la Polisi kufika
katika kijiji cha Mbimba kitongoji cha Isinizya wilayani Mbozi na
kumkuta mtoto huyo akiwa hoi bin taaban.
Wakati mtoto huyo akitolewa ndani ya nyumba alimofungiwa, wazazi
wake wote hawakuwepo nyumbani, na ikaelezwa kuwa mama yake mzazi alikuwa
shambani, ambapo alifuatwa na alipoletwa alidai kuwa mwanaye alizaliwa
akiwa na uzito mdogo na baadaye alielezwa hospitalini kuwa mtoto huyo ni
mlemavu wa akili.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ahamed Namohe amesema kuwa matukio ya
ukatili wa watoto wilayani mwake ni makubwa na kwamba kufichuliwa kwa
matukio hayo kunatokana na elimu ya kupinga ukatili huo ambayo imeanza
kutolewa wilayani Mbozi kwa kushirikiana na kituo cha haki za binadamu.
Mama mzazi wa mtoto huyo ameshikiliwa katika kituo cha Polisi cha
Vwawa wilayani Mbozi akisubiri kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na
ukatili huo.
Post A Comment: