Watu watatu kati ya wane, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka 12, ikiwamo la
kujipatia dola za Marekani 1,000 (zaidi ya sh. milioni mbili) kwa
kutumia jina la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Tuhuma zingine ni kula njama, kughushi barua za kampuni 12 ikiwamo IPP Media.
Mshtakiwa wa kwanza Issa Awadh (27) maarufu kama TRA Mwenge,
alisomewa mashitaka yake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili anakodaiwa
kulazwa kwa ajili ya matibabu.
Washtakiwa wengine, fundi mihuri Nicolaus Obado (32), Mtangazaji
Hamis Katembo (37) na mfanyabiashara Wakati Mungi (51) walisomewa
mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.
Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi na Pamela Shinyambala.
Shinyambala alidai kuwa kati ya Machi 10 na 17, mwaka huu, mahali
tofauti wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, wakiwa na wenzao ambao
hawakuwapo mahakamani, walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha
isivyo halali.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa kati ya Machi 10 na 17, mwaka
huu mahali tofauti wilayani Ilala, washtakiwa wote kwa pamoja
walijitambulisha kwamba ni watumishi wa umma kwa kutumika jina la Waziri
Mkuu, Majaliwa, huku wakijua ni kinyume cha sheria.
Ilidaiwa katika shitaka la tatu, siku na tarehe ya shtaka la pili,
washtakiwa kwa pamoja walighushi barua iliyoonyesha kutoka ofisi ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, ikimwelekeza mkurugenzi wa Kampuni ya
Usangu Logistic Ltd kuingiza Sh. milioni 25 katika akaunti ya TRA.HR.
MWENGE ili kupata punguzo la kodi.
Upande wa Jamhuri ulidai katika shitaka la nne, siku, tarehe na
mahali pa tukio la pili, kwa pamoja walighushi barua kutoka ofisi ya
rais, ikimwelekeza Mkurugenzi wa Kampuni ya Bakhresa Ltd kuingiza Sh.
milioni 25 katika akaunti iliyoko benki ya ABC kupitia akaunti ya
TRA.HR.
MWENGE.
Shinyambala alidai kuwa katika shtaka la tano, siku, tarehe na
mahali pa tukio la nne, washtakiwa walighushi barua kutoka ofisi ya Rais
ikimwelekeza Mkurugenzi wa IPP Media kuingiza Sh. milioni 25 katika
akaunti iliyopo benki ya ABC kupitia akaunti ya TRA.HR.MWENGE.
Shtaka la sita, tarehe na mahali pa tukio la tano, washtakiwa kwa
pamoja walighushi barua kutoka ofisi ya Rais ikimwelekeza Mkurugenzi wa
Kampuni ya Oil Com kuingiza Sh. milioni 25 katika akaunti iliyopo benki
ya ABC kupitia TRA.HR.MWENGE.
Shitaka la saba, tarehe na mahali pa tukio la sita, washtakiwa wote
kwa pamoja walighushi barua kutoka ofisi ya rais ikimwelekeza
Mkurugenzi wa Gapco Limited kuingiza Sh. Milioni 25 katika akaunti
iliyopo benki ya ABC kupitia TRA.HR.MWENGE.
Wakili huyo alidai katika shitaka la nane na la tisa, tarehe na
mahali pa tukio la saba, washtakiwa kwa pamoja walighushi barua kutoka
ofisi ya rais ikiwaelekeza kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Kampuni ya
Lake Oil Tanzania Limited, Puma Limited, kuingiza Sh. milioni 50 katika
akaunti iliyopo benki ya ABC kupitia TRA.HR. MWENGE ili kampuni hizo
zipate punguzo la kodi.
Ilidaiwa katika shitaka la 10, Machi 17, mwaka huu katika ofisi ya
kampuni ya Usangu Logistics Limited, washtakiwa waliwasilisha barua ya
kughushi kutoka ofisi ya Rais ikimwelekeza mkurugenzi wa kampuni hiyo
kuingiza Sh. milioni 25 benki ya ABC kupitia akaunti yenye jina la
TRA.HR. MWENGE ili kupunguziwa kodi.
Shitaka la 11, ilidaiwa kuwa Machi 10, katika ofisi ya TSN
Foundation, kwa nia ya kutenda kosa washtakiwa walijipatia Dola za
Kimarekani 1,000 kutoka kwa Farough Ahmed maarufu kama Bagozah kwa lengo
la kumdhamini Issa Awadh ama Charles Mwamunyange masomoni nchini
Marekani.
Washtakiwa walikana mashitaka hayo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Upande wa Jamhuri uliomba mahakama kuzuia dhamana dhidi ya
washtakiwa kwa kuwa wakitoka nje wataingilia upelelezi wa kesi hiyo.
Hakimu Simba alikubaliana maombi ya Jamhuri kesi hiyo itatajwa Aprili
12, mwaka huu na aliagiza upelelezi kukamilishwa haraka.
Post A Comment: