KUTOKANA na hali ya joto iliyopo jijini Dar es Salaam, Askofu wa
Huduma ya Good News for All, Charles Gadi amefanya maombi kuomba mvua
katika ukumbi wa Idara ya Habari, Maelezo mara baada ya kuzungumza na
waandishi wa habari.
Maombi hayo yaliyofanyika kwa nusu saa, yaliwashirikisha waandishi wa
habari na wachungaji mbalimbali wa huduma hiyo. Katika maombi hayo
yaliyofanyika jana, jijini humo, Askofu Gadi alisema hali ya hewa
imekuwa ya joto kubwa kama ilivyotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA).
Alisema hali hiyo imesababisha familia na ndoa kukosa raha na
kushindwa kuzaliana kama ilivyoelezwa katika Biblia kwamba wazae waijaze
dunia.
‘’Wanandoa wanakosa raha, watu wanalala nje kwa sababu ya joto kali
lililokuwepo. Mwaka jana katika kipindi hiki cha Pasaka kulikuwa na mvua
kubwa zilizosababisha mafuriko lakini ni tofauti na mwaka huu, hivyo
tuombee mvua,’’ alisema.
Alisema inapaswa kuendelea kuomba ili watu waweze kuishi kwa amani na
kwamba endapo watu hawataomba, inawezekana kusiwe na mvua za masika
kama walivyozoea.
Post A Comment: