IKIWA bila ya nyota wake tisa, wawakilishi wa Tanzania katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga jana walianza kambi kujiandaa
kwa michezo ya Kombe la FA, Ligi Kuu ya Tanzania Bara na ule wa
kimataifa dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Iliingia kambini baada ya mazoezi ya asubuhi yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Polisi Ufundi, Kurasini.
Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha msaidizi wa Yanga, Juma
Mwambusi alisema kikosi chake kimeingia kambini na wachezaji tisa ndio
wanaokosekana, wakiwemo saba ambao ni wagonjwa na wengine wakiwa kwenye
vikosi vyao vya timu za taifa.
Wanaoksekana katika kambi hiyo wametajwa kuwa ni Mbuyu Twite, Donald
Ngoma, Malimi Basungu, Saidi Juma `Makapu’, Geofrey Mwashiuya, Simon
Matheo na Benedicto Tinocco.
Tambwe na Niyonzima pia hawako kutokana na kukabiliwa na majukumu katika timu zao za taifa.
“Lakini wachezaji wetu wa kimataifa kama Amisi Tambwe (Burundi) na
Haruna Niyonzima (Rwanda) hatutakuwa nao kwa vile wapo kwenye timu zao
za taifa,” alisema Mwambusi.
Aliongeza kuwa, maandalizi yanaendelea vizuri huku akisema ari ya
kikosi chake ni kubwa na dhamira ya uongozi ni kuona Yanga inafanya
vizuri katika mashindano yote inayoshiriki.
“Tuna imani tutafanya vizuri kwani mpaka sasa tuna rekodi nzuri
kwenye mashindano tunayoshiriki,” alisema bila kutaja mahali ilipo kambi
yao, lakini ikiaminika ni moja ya hoteli za kifahari jijini Dar es
Salaam.
Yanga wanaingia kambini wakijiandaa na wiki ngumu zaidi kwani, kwani watacheza mechi nne za mashindano matatu ndani ya siku 10.
Kesho wataanza kwa kumenyana na Ndanda FC ya Mtwara katika hatua ya
16 Bora ya Kombe la FA, kabla ya kucheza mechi mbili mfululizo za Ligi
Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera Aprili 3 na
dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro Aprili 6.
Siku tatu baadaye mabingwa hao wa soka nchini watamenyana na Al Ahly
ya Misri katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa
barani Afrika.
Post A Comment: