ASKARI wa Kikosi cha Zimamoto, Manispaa ya Shinyanga wamenusurika
kipigo kutoka kwa wananchi wa mtaa wa Banduka, kata ya Ndala mjini hapa,
baada ya kuchelewa kufika kwenye tukio la nyumba kuungua moto ikiwa na
watoto ndani yake.
Baadhi ya mashuhuda walidai kuwa moto huo ulianza kuwaka kwenye
nyumba ya Azizi Abdallah, saa 2:00 asubuhi na uliunguza baadhi ya vitu
kwenye nyumba hiyo ambayo wanaishi wapangaji pekee kwa kile
kinachosadikiwa kuwa ni hitilafu ya umeme ambayo imekuwa ikijitokeza
mara kwa mara.
Mmoja wa walioshuhudia, Onesmo Shija, alisema wapangaji wote walikuwa
wamekwenda makazini na kubaki watoto ambapo saa 2:00 aliona moshi
ukifuka kwenye madirisha huku watoto wakipiga kelele, ndipo
walipokusanyika na kuanza kuuzima na kuwanusuru kifo watoto hao.
Shija alisema baada ya wananchi kutoa taarifa mapema kwa kikosi
hicho, walichelewa kufika na walipofika tayari moto ulikuwa umeshazimwa
ndipo wananchi walipopandwa hasira na kuanza kuokota mawe na
kuwashambulia lakini mwenyekiti wa mtaa aliwazuia.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Terege Nyankangara alisikitishwa na kikosi
cha Zimamoto kuchelewa kufika eneo la tukio na kueleza uchelewaji huo
ulitaka kuhatarisha amani. Hata hivyo, Nyankangara aliwaasa wananchi
wake kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Askari wa kikosi cha Zimamoto, Omari Magea alikiri wananchi hao
kutaka kuwashambulia kwa mawe na alishukuru Mwenyekiti wa mtaa kuwezesha
kurejesha amani. Alisema kilichowachelewesha ni uhaba wa vitendea kazi.
Post A Comment: