Siasa imeshika hatamu kwa sasa katika vijiwe vingi nchini Tanzania,
mbali na majadiliano kuhusu hatma ya siasa Zanzibar na ushindi wa Dkt
Shein, sasa hivi kuna mivutano ya hapa na pale ati katika muungano wa
vyama vya upinzani UKAWA, Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA,
inavinyonya vyama vingine hususani chama cha wananchi CUF.
Aliyewahi kuwa naibu katibu mkuu CUF Tanzania bara na mchambuzi wa
siasa, Julius Mtatiro ametoa mtazamo wake na kufafanua kauli hizi kama
ni kweli CUF inapunjwa ama la, kupitia ukurasa wake wa Facebook kaamua
kuyaandika yafuatayo.
Kuna mjadala mkubwa umeendeshwa jana wadau wengi wakihoji kwa nini
CUF haikuachiwa umeya wa jiji wakati yenyewe ndiyo ina madiwani wengi?
Wengine wamefika mbali na kutamka kuwa CUF inamezwa na CHADEMA. Kama mtu
nayefuatilia kwa ukaribu masuala ya siasa za nchi, za vyama n.k.
ukiachilia mbali kuwa kwangu karibu na viongozi wa UKAWA na UKAWA
yenyewe, niliona nisaidie kutoa ufafanuzi ufuatao;
Kwanza, chama chenye madiwani wengi katika jiji la DSM ni CHADEMA, huwenda madiwani wa chama hicho ni wengi karibia mara mbili ya wale wa CUF.
Pili, utaratibu wa kutoa meya wa manispaa au jiji ni mchakato wa
maridhiano baina ya vyama vya UKAWA. Hatujasikia popote viongozi wa
chama chochote cha UKAWA wakilalamika kuwa hawakutendewa haki kwenye
michakato hiyo, kwa hiyo nadhani aliyegombea alipitishwa na pande zote.
Tatu, katika jiji CUF imeachiwa itoe mgombea wa Unaibu Meya wa JIJI
atakayemsaidia Meya. CUF imeshamteua Mhe. Mussa Swedi Kafana, diwani wa
kata ya Kiwalani iliyoko jimbo la Segerea.
Nne, utaratibu wa kumchagua Naibu Meya wa Jiji hufanyika mara baada
ya uchaguzi wa Meya wa Jiji. Naibu Meya hapigiwi kura na kusanyiko la
madiwani wote wa jiji bali yeye huchaguliwa kwenye kikao rasmi cha
Baraza la Halmashauri ya Jiji la DAR ambalo huwa na wajumbe kama 25
hivi, wajumbe hao wanatokana na uwakilishi wa madiwani wachache kutoka
kila Manispaa zinazounda jiji, uchaguzi huu wa Naibu Meya wa Jiji bado
haujafanyika.
Tano, watu wengi hupenda kuonesha namna gani ambavyo hakuna USAWA
ndani ya UKAWA na namna gani CHADEMA imevipiku vyama vingine na wengi
huishauri CUF na NCCR visikubali na ikiwezekana vijitoe, Ukweli ni kuwa
ndani ya UKAWA kuna changamoto zake na kadri muda utakavyokuwa unasonga
zitakuwa zinajitokeza n.k. Jambo la msingi ni viongozi wa UKAWA
kuendelea kuzishughulikia ili zisijirudie.
Sita, mafanikio ya vyama vya upinzani vya Tanzania leo hii yanatokana
na UKAWA na kama kuna chama kimoja kitajitia “wazimu” kijitoe UKAWA
kitajuta. Siasa zimebadilika sana na bila muungano “mnapigwa tu”.
Changamoto zilizomo ndani ya UKAWA ni chache sana kulinganisha na faida
za moja kwa moja na zisizoonekana ambazo vyama vilivyomo na hata
wananchi wanavyonufaika kidemokrasia.
Saba, hata siku moja, Vyama vinavyoongoza dola haviwezi kufurahia
muungano wa vyama vya upinzani, kokote kule! Wapinzani wanapoungana ni
“kitisho” kikuu cha anguko la vyama dola. Ndiyo maana siyo ajabu kukuta
vijana wanashinda mitandaoni wakieleza namna gani UKAWA haipaswi
kuendelea. Kwa tunaoamini kwenye demokrasia ya kweli tunaona ni heri
UKAWA yenye changamoto kuliko utengano wa vyama utakaoirahisishia CCM
kazi ya kutawala.
Post A Comment: