WAKAZI wa Machinjioni wilayani Kibaha mkoani Pwani, wameiomba
Halmashauri ya Mji wa Kibaha, kutekeleza agizo la Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi la kumaliza mgogoro wa
ardhi kwenye eneo lao. Walisema eneo lao hilo lina mgogoro tangu mwaka
2010.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, moja ya wananchi wa
eneo Hilo, Said Tekelo alisema kuwa suala la mgogoro walilikabidhi kwa
Lukuvi, ambaye aliipa Halmashauri ya Mji Kibaha miezi miwili kumaliza
mgogoro huo ili haki zao zipatikane.
Tekelo alisema kuwa katika mgogoro huo, wananchi hawatakiwi
kuendeleza maeneo yao tangu mwaka jana. Alisema hadi sasa hawajui hatma
ya maeneo yao. “Sisi tunachotaka ni kulipwa na kuonyeshwa maeneo mengine
kwa ajili ya kuishi, kwani tayari wananchi 41 walivunjiwa nyumba zao
mwaka 2012 na baada ya hapo hakuna kilichofanyika.
Wametusimamisha kupata maendeleo kwa muda wote huo hakuna aliyelipwa
chochote,” alisema Tekelo. Alisema kuwa wanashangazwa kuona Halmashauri
imepima maeneo hayo na kuweka alama za mpaka kwenye maeneo yao, bila
kusema chochote kwenye eneo hilo, ambalo lina wananchi 360 na lina
ukubwa wa zaidi ya hekari 60.
“Tunamwomba Waziri Lukuvi atusaidie kwani tunaona agizo lake
halijafanyiwa kazi na muda aliopanga wa miezi miwili, tunaona hakuna
kinachoendelea, kwani halmashauri bado hawajatekeleza agizo lake la
kuutatua mgogoro huu,” alisema Tekelo
Post A Comment: