Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein amemteua
Balozi Seif Ali Idd kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 39 (2) cha
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Dk Shein amemteua Balozi Idd ambaye
alikuwa na wadhifa huo hata kipindi kilichopita.
Uteuzi wa Balozi Idd aliyezaliwa Februari 23, mwaka 1942, ulianza
jana ikiwa ni siku nne tangu kuapishwa kwa Shein kuwa Rais wa Zanzibar.
Balozi Idd anakuwa mtu wa pili kuteuliwa na Dk Shein baada ya
kuteuliwa kwa mwanasheria mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said mwishoni mwa
wiki.
Dk Shein sasa atakuwa na wakati mgumu wa ama kumteua au kutomteua
Makamu wa Kwanza wa Rais ili kukidhi matakwa ya Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK) kwani hakuna chama cha upinzani kilichokidhi vigezo vya
kushirikishwa katika kuunda Serikali.
Post A Comment: