ALIYEKUWA Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa zaidi ya miaka 20 sasa,
Pandu Ameir Kificho, ameng’olewa katika nafasi hiyo baada ya kushindwa
katika kura za kuwania awamu nyingine ya uongozi wa baraza hilo.
Badala yake wajumbe wateule wa Baraza la Wawakilishi, wamemchagua
Zubeir Ali Maulid, kuwa Spika mteule wa baraza hilo, baada ya kupata
kura 55 na kumuacha kwa mbali Kificho aliyeambulia kura 11 katika
uchaguzi uliofanyika jana katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar.
Aidha katika uchaguzi huo ambao wawakilishi 72 walipiga kura, Janeth
Nora Sekihola ambaye ni hakimu mstaafu akipata kura 4 wakati kura mbili
ziliharibika.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuangushwa
katika uchaguzi huo, Kificho alisema amekubali kushindwa na yupo tayari
kutoa ushirikiano akitakiwa kufanya hivyo.
“Hiyo ndiyo demokrasia, nimekubali kushindwa na nipo tayari kutoa
ushirikiano mkubwa nikitakiwa kufanya hivyo kwa sababu ni ukweli kwamba
ninao uzoefu mkubwa katika nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 20,” alisema.
Naye Spika mteule wa baraza hilo, Maulid alisema anakabiliwa na
changamoto kubwa ya kuleta maendeleo na mabadiliko makubwa katika chombo
hicho ambacho ni moja ya mihimili ya dola katika utekelezaji wa
majukumu yake.
Post A Comment: