Klabu ya Simba imesema kuwa Kocha Mkuu aliyepita Dylan Kerr
aliwadekeza wachezaji wa timu hiyo kiasi cha kushindwa kufanya majukumu
yake ipasavyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa klabu hiyo Haji
Manara alisema kuwa kocha huyo alikuwa akipangiwa hata kikosi na
wachezaji wenyewe.
Manara alisema hayo kufuatia baadhi ya wadau wa soka kuanza kuhoji jinsi kocha wa sasa Jackson Mayanja alivyokuwa mkali.
Kocha huyo aliwasimamisha wachezaji wawili wa timu hiyo Hassan
Isihaka ambaye tayari ameshamaliza adhabu yake na Abdi Banda kutokana na
kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
"Kocha alikuwa akipangiwa kikosi na wachezaji wenyewe, na siku
akipanga mwenyewe mmoja akikunja sura kuonekana kuwa amekasirika basi
anampanga hata kama hayuko fiti," alisema Manara.
Mbali na hayo, Afisa Habari huyo alisema chini ya Kerr, wachezaji
walikuwa akigomea mazoezi na kocha hakuwa na uwezo wa kuwaambia lolote.
"Siku moja nilikuwa na timu kocha alinifuata na kuniambia wachezaji
wamegomea mazoezi kwa sababu mishahara imechelewa. Mimi niliwafuata na
kuwaambia kuwa pesa zao watapata zimechelewa kwa sababu wadhamini
wamechelewesha kwa sababu za kiofisi tu, nikawaambia kama mtu hataki
mazoezi kwa sababu hii basi achukue begi lake aondoke. Walirejea
mazoezini," alisema afisa huyo.
Alisema kwa sasa Simba imempata kocha ambaye anajua majukumu yake na ndiyo maana unaona haya yote yanatokea.
"Nidhamu imekuwa juu ndani na nje ya uwanja, Simba sasa inacheza dakika zote 90, inaweza kufunga goli dakika yoyote," alisema.
Post A Comment: