Klabu ya Simba imezindua wiki ya timu hiyo kuelekea tamasha kubwa la Simba Day litakalofanyika Agosti 8 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya EAG ambao ni washirika wa Simba, Iman Kajura alisema wamezindua Wiki ya Simba ili kurudisha shukrani kwa jamii kwani soka si kucheza uwanjani tu bali kufanya mambo yenye tija kwa jamii.
Kajura alisema kesho Jumatano itazinduliwa kampeni ya mtaa kwa mtaa Dar es Salaam nzima na watatembelea matawi yote ya klabu hiyo.
Alisema Agosti 3 watawatembelea wachezaji wa zamani wa klabu hiyo huku Agosti 4 wakitoa misaada kwa vituo mbalimbali vya watoto yatima.
"Wiki ya Simba tuliizindua mwaka jana na ilifanyika kwa mafanikio makubwa ikiwemo kuchangia damu na sasa tunafanya tena mwaka huu ili kurudisha kwa jamii."
"Timu itarejea Agosti 5 kutoka Afrika Kusini ilikoweka kambi na Agosti 6 itafanya kliniki ya watoto na kugawa mipira pia kutembelea wadhamini na kuchangia masuala ya upasuaji wa moyo kwa watoto katika Hospitali ya Muhimbili," alisema Kajura.
Kajura alisema Agosti 7 wachezaji watapata fursa ya kuongea moja kwa moja na mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.
Alisema Agosti 8 watazindua rasmi zawadi kwa wachezaji bora wa Simba kwa kipindi chote (All of Fame), huku pia wakitoa zawadi kwa mchezaji aliyecheza mechi zote za timu hiyo kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita ambaye ni Mohammed Hussein'Tshabalala.
Post A Comment: