Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa zinazotokana na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.
Mradi huo utakaogharimu Sh8 trilioni, unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 10,000 wakati wa ujenzi wa bomba.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Juliana Pallangyo, amesema ujenzi wa bomba hilo unaotarajiwa kuzinduliwa Agosti 5, mwqaka huu, utatoa wigo mpana wa shughuli za kiuchumi.
Amesema hakuna sababu ya watu kusubiri baadaye na kutoa lawama kwa serikali kuwa watu wa nje wananufaika na mradi huo ilhali wazawa wapo.
"Nitoe wito kwa watanzania wajikusanye katika vikundi vyao na kupitia utaratibu rasmi kutafuta shughuli za kufanya katika mradi huu," amesema.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Watoa Huduma wa Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim, amewahamasisha watoa huduma katika sekta hiyo kujitosa kwa haraka na kuchukua fursa zilizopo.
Amesema hadi sasa watoa huduma wa Tanzania waliojisajili kwenye jumuiya hiyo wamweonyesha uwezo na utayari wa kushiriki kikamilifu kwenye mradi huo.
Amesema: "Tunaamini fursa nyingi zitafunguka baada ya ujenzi kuanza. Wapo watoa huduma wa ujenzi, uandisi, ununuzi, uwezeshi pamoja na huduma za bima, benki, kisheria, ulinzi, chakula na dharura."
Post A Comment: