WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema serikali imebaini kwamba watumishi wa sekta ya ardhi katika kipindi cha awamu tofauti wamechangia kwa kiwango kikubwa migogoro ya ardhi kutokana na vitendo vyao vya utapeli.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika mwendelezo wa kusikiliza mashauri mbalimbali ya migogoro ya ardhi, kutoka kwa wananchi wa Ilala, Temeke na Kinondoni.
Waziri Lukuvi alisema watumishi wa ardhi katika kipindi hicho, waliifanya sekta hiyo kama sehemu ya kufanyia utapeli na kujipatia fedha.
Alisema katika uchunguzi wao, wamebaini kwamba watumishi hao walikuwa wakiwapimia wananchi viwanja na kuwapatia hati na leseni feki na wakati mwingine kutoa viwanja kwa zaidi ya mtu mmoja.
Alisema watumishi wengi waliokuwa wakifanya hivyo, wengi wao hawako tena kazini na baadhi waliopo wameshaanza kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Tumebaini kwamba matatizo na migogoro mingi ya ardhi ilikuwa inasababishwa na maofisa wa ardhi katika serikali ya awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu. Watumishi hawa walikuwa wanatumia mwanya walio nao kutengeneza hati na leseni feki,” alisema Lukuvi.
“Walikuwa hawatendi kazi kwa mujibu wa sharia. Wapo wananchi ambao walidhulumiwa viwanja vyao na wengine wakapewa ambavyo si vya kwao. Wamiliki halali walinyang`anywa wakapewa wasio wamiliki halali na hata maeneo ambayo hayakustahili kupewa wananchi, wao walitengeneza ofa feki na kuwapatia watu na wakati mwingine walikuwa wanashirikiana na matapeli wengine wa kawaida.
“Kwa hiyo kumekuwa na migogoro mikubwa sana na watu wanaishi na madukuduku yanayosababishwa na maofisa wasio waamini kwa kipindi kirefu.”
Alisema maofisa hao walikuwa wanafanya utapeli huo nchi nzima na kwamba mkoa wa Dar es Salaam ndio unaongoza kwa wananchi wake kupewa hati feki.
Lukuvi alisema moja ya mbinu zilizokuwa zikifanywa na maofisa hao ni kutembelea maeneo ya ardhi wanayomiliki wananchi na yale ya wazi halafu wanatengeneza hati feki.
“Walikuwa wakigundua kwa mfano hati imetengenezwa mwaka 1990 wao walichokuwa wakifanya ni kutengeneza hati ya miaka ya nyuma kidogo na walikuwa wakitengeneza wanazidumbukiza kwenye majani ya chai ili zionekane za zamani, kwa hiyo hati nyingi zinazoonekana za zamani ndiyo feki,” alisema Lukuvi.
Alisema kazi inayofanywa na serikali kwa sasa ni kuhakikisha wananchi wote waliomilikishwa maeneo isivyo halali wananyang`anywa na kurudushiwa wamiliki halali.
Alisema tayari serikali imeshaanza kufanya kazi hiyo na kwamba mpaka sasa wananchi waliobainika kutapeliwa maeneo yao serikali imelazimika kuwapatia maeneo mengine kwa gharama nafuu kwa ajili ya kuwafuta machozi.
Alisema kwa Dar es Salaam pekee mpaka sasa wananchi ambao wamekwisha patiwa maeneo ambao walibainika kutapeliwa ni zaidi ya 700 na kwamba kazi ya kuwabaini walioathirika bado inaendelea.
Pia alisema kuna hati ambazo zilitolewa na maofisa hao ambao serikali imelazimika kuzifuta.
“Awamu ya tano imeamua kuwafuta machozi waliotendewa udhalimu na watumishi wa serikali wa kipindi hicho, inasikitisha sana sehemu nyingine watendaji walikuwa wakipima maeneo zaidi ya mara moja, unakuta eneo linatosha watu 100, lakini wao walikuwa wanatoa hati hata zaidi ya 300. Watumishi hawa walikuwa hawajali na hawakuwa na huruma kabisa,” alisema Lukuvi.
“Wakati mwingine kwa kushirikiana na matapeli wengine wasio watumishi wa serikali, walikuwa wakikuta kama kuna mtu mwenye eneo lake ameweka Wamasai kwa ajili ya ulinzi, walikuwa wanawatishia, wanawatoa na kuweka walinzi wao na wanatapeli moja kwa moja.”
Lukuvi alisema serikali kwa sasa imejiandaa kuhakikisha kwa yeyote atakayeingia tena katika mchezo huo wa utapeli hasalimiki kutokana na mtandao waliouweka na kwamba tayari wana taarifa za matapeli wengine wasio watumishi wa umma ambao wamekuwa wakifanya mchezo huo.
Post A Comment: