BAADA ya kutoonekana jukwaani kwa muda mrefu, hatimaye Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ameibuka na kueleza kuwa hakuna shida yoyote kwa Rais John Magufuli kuendelea kurekebisha makosa yaliyofanywa na serikali za awamu zilizopita
Kinana aliadimika jukwaani tangu Machi, mwaka huu, lakini baadaye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kiongozi huyo (Kinana) amekwenda kwenye matibabu.
Kinana aliyasema hayo jana Mkanyageni, Muheza mkoani Tanga wakati alipopewa nafasi ya kuzungumza na wananchi waliojitokeza kwa maelfu kumsikiliza Rais Magufuli.
Akifafanua kauli yake, alisema kuwa jitihada zinazofanywa na serikali ya sasa ya awamu ya tano katika kurekebisha makosa, ni sahihi na hakuna tatizo lolote kufanya hivyo kutokana na ukweli kuwa zote (serikali zilizopita na ya sasa) ni za CCM.
Kabla serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli kuingia madarakani Novemba 5, 2015, wakuu wastaafu waliotangulia kabla yake ni Jakaya Kikwete wa awamu ya nne (2005-2015) na Benjamin Mkapa wa awamu ya tatu (1995-2015). Hata hivyo, katika hotuba yake hiyo, Kinana hakutaja moja kwa moja jina la kiongozi yeyote aliyemtangulia Magufuli.
Akifafanua juu ya jambo hilo lililoashiria kukiri kwake juu ya baadhi ya madudu yaliyojitokeza katika awamu zilizopita, Kinana alisema kama kuna makosa yaliyofanywa na viongozi wa awamu zilizopita hakuna shida kwa sababu hata anayerekebisha sasa pia ni mwana CCM.
Alisema kumekuwa na malalamiko kuwa rais wa awamu ya tano (Magufuli) anaichokonoa serikali ya awamu ya nne, jambo alilodai kuwa kwake haoni kama ni la ajabu kwa sababu yote yanafanywa na wanaCCM.
“Lakini kama aliyeharibu ni mwana CCM, anayekosoa na anayerekebisha ni mwana CCM, mimi sioni tatizo. Hivyo tuachane na kulalamika… tufanye kazi,” alisema Kinana.
Aidha, alisema kuna mambo ambayo hayakufanywa au kuchukuliwa uamuzi kwa haraka katika kipindi kilichopita, lakini kwa sasa yanafanyika kwa haraka ili kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Tangu kuingia kwake madarakani, Serikali ya Rais Magufuli imekuwa ikipambana kivitendo katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi na hadi sasa, tayari kuna kesi kadhaa zimefunguliwa na baadhi ya watuhumiwa kupandishwa kizimbani.
Aidha, Rais Magufuli amekuwa akiwaondoa kwenye nafasi zao watu mbalimbali waliopewa dhamana za kuongoza taasisi za umma na kwenda kinyume cha matarajio au kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali. Amekuwa akifanikisha hilo kwa kutumia kaulimbiu yake maarufu ya ‘utumbuaji majipu’.
JPM AZIDI KUMWAGA CHECHE
Kwa upande wake, Rais Magufuli akiwa Mkanyangeni, alisema ataendelea kuwatumbua mafisadi, wakiwamo waliokimbilia CCM ili kuficha maovu yao.
“Waliojificha ndani ya CCM kumbe ni mafisadi nitawatumbulia huko huko. Ni mara kumi uwe na Chadema au CUF ambaye ni mzuri, anayetekeleza ilani ya CCM kuliko kuwa na CCM ambaye ni ovyo… anahujumu mali za Watanzania wengine,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, akizungumza wakati akiwa katika eneo la Hale, Rais Magufuli alisema Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Robert Gabiel, anafanya kazi nzuri kwa kuwashirikisha wananchi wa eneo hilo kujenga vyumba vya madarasa kwa gharama nafuu na kufanikiwa kujenga vyumba vingi.
“Wakiona umepanda, wasikuonee wivu. Umetumia fedha kutoka Tamisemi kujenga vyumba vya madarasa kwa kutumia mafundi wa eneo husika. Kama kuna nafasi za juu huyu nitampa, hata RC amezungumza vizuri dhidi yako,” alisema Rais na kuongeza:
“Nimeanza kumsifia, ila sifa ninazokumwagia siyo zangu bali ni za wananchi na viongozi wengine. Tumezoea kusubiri kusifia watu wakishakufa, utasikia wakisema kuwa pengo lake halizibiki, lakini akifa kumbe mnaziba siku hiyo hiyo,” alisema Rais Magufuli wakati akimwelezea Mkuu wa Wilaya hiyo na kuibua vicheko kwa wananchi waliokuwapo.
Rais Magufuli yuko katika ziara ya kikazi mkoani Tanga na kesho anatarajiwa kuzindua mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga lenye urefu wa kilomita 1,425, akiwa na mgeni wake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Post A Comment: