WAKATI shauku ya Watanzania ikiendelea kuwa juu kuhusiana na hatima ya mazungumzo yanayoendelea baina ya Serikali na kampuni ya Barrick juu ya biashara ya madini ya migodi yake nchini, ikiwamo madai ya kodi ya Sh. trilioni 420imebainika kuwa kiasi hicho cha fedha ni kikubwa na kinaweza kufanya mambo ya manufaa kwa wakati mmoja.
Jumatatu iliyopita, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitoa taarifa juu ya kuanza kwa majadiliano baina ya Kamati Maalumu iliyoundwa na Rais John Magufuli na Wawakilishi kutoka kampuni ya Barrick Gold Corporation juu ya biashara ya madini yanayochimbwa na migodi ya kampuni hiyo nchini.
Hatua hiyo ilifikiwa ikiwa ni siku chache baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuitaka kampuni hiyo inayomiliki hisa nyingi za kampuni ya migodi ya Acacia kulipa dola za Marekani bilioni 190 (Sh. trilioni 420), ikiwa ni fedha zitokanazo na malimbikizo ya kodi tangu mwaka 2000 pamoja na adhabu.
Uchambuzi uliofanywa na gazeti la Nipashe kuhusiana na fedha hizo, umebaini kuwa Watanzania wana kila sababu ya kutanguliza sala na maombi kwa kamati iliyoundwa na Rais, ikiongozwa na Waziri wa Sheria na Katiba, Prof. Palamagamba Kabudi, ili mwishowe ifanye vizuri na kufanikisha kulipwa kwa fedha hizo ili kutimiza dhamira ya Rais Magufuli kuona kuwa taifa linanufaika na rasilimali hiyo.
Aidha, uchambuzi huo umebaini kuwa endapo fedha hizo zitapatikana, mambo 10 makubwa yanaweza kufanyika kwa kiwango cha juu.
Baadhi ya mambo hayo, kwa mujibu wa uchambuzi wa gazeti la Nipashe, ni pamoja na kuwezesha ununuaji wa gari aina ya Noah kwa kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18; kujenga mtandao mkubwa zaidi wa barabara za lami; kugawa mitaji ya biashara ya kiwango cha zaidi ya milioni 10 kwa kila mwanamke nchini; kusomesha bure idadi kubwa ya wanafunzi wa elimu ya juu na pia kuwapo na ‘jeuri’ ya kuwanywesha maziwa walau lita tatu kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 15 na huduma hiyo kudumu kwa miaka mitano.
Aidha, fedha za kodi ya madini zikipatikana, taifa linaweza pia kufanya ‘kufuru’ ya kuwanunulia pikipiki na bajaji Watanzania wote; kujenga maabara zaidi za shule za sekondari; kununua mamilioni ya madawati; kutoa dawa bure kwa kila Mtanzania kwa miaka takribani 20 mfululizo na ‘kufuru’ nyingine itokanayo na jeuri ya fedha hizo, ni uwezo wa fedha hizo kuwanunulia bia wanaume wote, tena kwa kiasi cha kreti moja kila siku na kisha huduma hiyo kuweza kudumishwa kwa miezi saba mfululizo.
“Profesa Kabudi amesema kamati yake imejipanga vizuri kujadiliana na Barrick Gold Corporation juu ya madai ya Tanzania katika biashara ya madini ya kampuni hiyo hapa nchini na itahakikisha inasimamia maslahi ya Tanzania ipasavyo,” sehemu ya taarifa ya Ikulu ilieleza kuhusiana na kuanza kwa majadiliano hayo. Katika mazungumzo hayo, timu ya Barrick inaongozwa na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wake, Richard Williams.
Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kiuchumi aliiambia gazeti la Nipashe jana kuwa Watanzania wote wanatakiwa kuungana katika kuiombea kamati ya kina Kabudi ili iwezeshe kulipwa kwa kodi iliyotajwa na TRA.
“Kiukweli hizo fedha zinazotajwa ni nyingi sana. Kikieleweka katika mazungumzo na fedha hizo zikapatikana, serikali itakuwa na uwezo wa kufanya mambo mengi ya maendeleo kwa muda mfupi,” alisema mchambuzi huyo, kuelezea madai ya TRA ya Sh. trilioni 420 kwa kampuni ya Barrick.
Hivi karibuni, kamati mbili zilizoundwa na Rais Magufuli kuchunguza usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia) kwenda nje ya nchi katika makontena 277 yaliyoshikiliwa bandarini Dar es Salaam zilibaini upotevu mkubwa wa mapato uliotokana na tofauti ya taarifa zilizokuwa zikitolewa na uhalisia wa kaisi cha madini kilichokuwa kikisafirishwa.
1. NOAH MPYA KILA MTANZANIA
Katika uchunguzi wake, gazeti la Nipashe limebaini kuwa kwa wastani, bei ya gari moja aina ya Toyota Noah kwenye ‘show room’ nyingi jijini Dar es Salaam ni Sh. milioni 15.
Aidha, Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), makadirio ya idadi ya watu nchini kufikia mwaka 2016 yalionyesha kuwapo kwa watu milioni 50.14, kati yao wanaume wakiwa milioni 24.41 na wanawake milioni 25.73. Kwa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuelekea Oktoba 25, 2015, watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 18 nchini ni milioni 23.16.
Kwa sababu hiyo, endapo itaamuliwa kuwa Sh. trilioni 425 za kodi itokanayo na migodi itumike kuwanunulia Noah Watanzania wenye umri wa kuanzia miaka 18, maana yake kila mmoja atapata gari hilo moja na mengine takribani milioni 2 yatakosa wenyewe.
2. MITAJI KWA KINAMAMA
Kwa mujibu wa NBS, idadi ya wanawake nchini kufikia mwishoni mwa mwaka 2016 ni takribani milioni 26. Kwa sababu hiyo, endapo kodi ya makinikia kiasi cha Sh. trilioni 420 itaelekezwa katika kuwapa mitaji ya biashara wanawake wote nchini, maana yake kila mmoja wao atapata Sh. milioni 16.
3. WATOTO MAZIWA KILA SIKU
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto chini ya miaka 15 ni asilimia 48. Hivyo, katika idadi ya watu milioni 50.4 wanaokadiriwa kuwapo nchini, maana yake watoto wa umri chini ya miaka 15 ni sawa na milioni 24.
Endapo kodi ya makinikia Sh. trilioni 420 itatumika kuwanunulia maziwa watoto wa idadi hiyo kwa bei ya wastani wa Sh. 3,000 kwa lita moja, maana yake kila mmoja wao atakunywa maziwa lita tatu kila siku na huduma hiyo itadumu kwa miaka mitano. Mwaka mmoja ni sawa na siku 365.
4. BIA KRETI MOJA KILA MWANAMUME
Ingawa bei ya bia hutofautiana kulingana na chapa na eneo, lakini kwa wastani kila moja huuzwa Sh. 2,500 na hivyo kreti moja lenye bia 24 huwa sawa na Sh. 60,000. Aidha, kwa mujibu wa NBS, idadi ya wanaume nchini kufikia mwishoni mwa mwaka 2016 ni milioni 24. Kwa sababu hiyo, endapo kodi ya makinikia (Sh. trilioni 420) ingepatikana na kisha yote kugawiwa kwa wanaume nchini ili wanunulie bia, maana yake kila mmoja angepata kreti moja kwa siku na huduma hiyo ingedumu kwa miezi zaidi ya saba.
5. KILA MTANZANIA BOXER 5, BAJAJI 2
Katika maduka mengi ya vyombo vya moto jijini Dar es Salaam, pikipiki aina ya Boxer huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni mbili huku zile za miguu mitatu, maarufu kama bajaji, zikiuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 6.
Aidha, kwa takwimu za NEC katika uchaguzi mkuu uliopita, watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 18 nchini ni milioni 23.16.
Kwa sababu hiyo, endapo kodi ya makinikia kiasi cha Sh. trilioni 420 itapatikana na kutumika kuwanunulia pikipiki Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18, maana yake kila mmoja angepata Boxer tisa. Aidha, zingepatikana bajaji tatu kwa kila Mtanzania endapo fedha hizo zingetumika kununulia chombo hicho.
6. DAWA BURE HOSPITALINI
Katika mwaka huu wa fedha 2017/2018, Serikali imepanga kutumia Sh. bilioni 236 kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba kwenye hospitali za umma nchini kote. Kwa sababu hiyo, endapo bajeti hiyo ingeongezwa mara 100 ili kukidhi mahitaji ya dawa bure kwa ukamilifu kwa mwaka, maana yake zingehitajika Sh. trilioni 23.
Kwa hesabu hiyo, uchambuzi wa Nipashe ulibaini kuwa Sh. trilioni 420 za makinikia zingetosha kwa makadirio ya bajeti ya Sh. trilioni 23 kwa mwaka kuwatibu bure Watanzania kwa miaka takribani 20.
7. MAABARA ZA SEKONDARI
Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandika, Hussein Mpungusi, aliwahi kukaririwa Aprili 20, 2015, akisema kuwa walikamilisha ujenzi wa maabara mojawapo shuleni kwake kwa Sh. milioni 58.2.
Ikiwa fedha za kodi ya makinikia zitapatikana na (Sh. trilioni 420) na kuelekezwa katika ujenzi wa maabara za viwango walau mara mbili ya thamani ya maabara ya Sekondari ya Tandika, maana yake zitapatikana maabara za aina hiyo takribani 4,200,000.
8. MADAWATI
Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, aliwahi kukaririwa na Nipashe akisema kuwa wastani wa bei ya dawati moja linalokaliwa na wanafunzi watatu wa shule ya msingi katika jimbo lake ni Sh. 15,000.
Kwa sababu hiyo, endapo kodi inayohusishwa na makinikia kiasi cha Sh. trilioni 420 itapatikana na kuelekezwa katika kumaliza tatizo la madawati, maana yake yangepatikana madawati yenye thamani mara mia moja ya yale ya Singida Magharibi (Sh. milioni 1.5 kila moja) ya idadi inayofikia 280,000,000 na kumaliza tatizo hilo nchini kote na kisha mengine kuweza kusambazwa nchi nyinginezo barani Afrika.
9. MAGARI YA KUBEBEA WAGONJWA
Agosti 28, 2014, kulikuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa kampuni ya Biolands International ilikabidhi msaada wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Nissan Patrol kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela lenye thamani ya takriban Sh. milioni 76. Kwa sababu hiyo, ikiwa kodi ya makinikia (Sh. trilioni 420) itapatikana na kutumika kununulia ambulance za kisasa zenye thamani ya Sh. milioni 500 kila moja, maana yake taifa litapata magari mapya ya kubebea wagonjwa takribani 840,000 na hivyo kumaliza kabisa tatizo la ukosefu wa magari hayo, kuanzia katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa hadi za rufaa nchini kote.
10. MIKOPO ELIMU YA JUU
Katika uchunguzi wake, Nipashe iliwahi kubaini kuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayepata mkopo wa asilimia 100 hulipwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jumla ya Sh. 4,219,500 kwa mwaka. Mchanganuo wa mkopo huo kwa mwaka wote wa masomo ni Sh. 2,099,500 kwa ajili ya chakula na malazi, Sh. 200,000 ya vifaa, Sh. 620,000 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, ada Sh. milioni 1.3.
Kwa hesabu hizo, ikiwa kodi ya makinikia itapatikana na kuelekezwa katika kuwasomesha wanafunzi wa elimu ya juu kama wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini wanaolipwa asilimia 100, maana yake wanafunzi million mbili wangesomeshwa na fedha hizo kila mwaka na huduma hiyo ingedumu kwa miaka mitano. Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), wanafunzi wote nchini hawazidi 300,000.
MENGINEYO
Vyanzo mbalimbali vya Nipashe vinaeleza kuwa kipimo maarufu cha CT-Scan, aina ya Phillips huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 600 hadi bilioni moja. Hivyo, kama kodi ya makinikia itapatikana na kutumika kununulia mashine za vipimo hivyo, maana yake zinaweza kupatikana mashine 420,000 za thamani ya Sh. bilioni moja kila moja, hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa vipimo hivyo nchini.
Aidha, fedha za kodi ya makinikia zinaweza pia kujenga mtandao wa barabara safi za lami za urefu wa kilomita 420,000 ikiwa kila kilomita moja hujengwa kwa thamani ya Sh. bilioni moja. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, Chama Cha Mapinduzi kiliwahi kuahidi kuongeza mtandao wa barabara za lami wa umbali wa kilomita zaidi ya 4,000.
Aidha, kwa mujibu wa kikokotozi cha umbali cha mtandao wa Distancefrom, umbali wa barabara kutoka jijini Dar es Salaam hadi Bukoba ni kilomita 1,376.
Credit - Nipashe
Post A Comment: