Wakati idadi ya watu maarufu kutoka nje ya nchi wanaokuja kutazama vivutio vya utalii nchini ikiongezeka, mtandao wa kimataifa wa kibiashara umeitangaza Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika inayowavutia zaidi watalii.
Mtandao huo, SafariBookings.com ulifanya uchambuzi kwa kuchukua maoni ya watalii zaidi ya 2,500 waliotembelea nchi za Afrika na idadi kubwa waliitaja Tanzania kuwa bora kuliko nchi nyingine.
Hii ni mara ya pili kwa mtandao huo wa Marekani kuitaja Tanzania kama nchi ya kwanza inayowavutia zaidi watalii. Mara ya kwanza ilikuwa 2013.
Sifa kubwa iliyoipa hadhi ya juu Tanzania ni kuwa na eneo kubwa lenye wanyamapori na misitu. Nchi nyingine zilizoshika nafasi ya juu ni Zambia na Kenya.
Wakati mtandao huo ukiitaja Tanzania kuwa eneo bora la utalii, watu maarufu kutoka mataifa makubwa duniani wameendelea kumiminika nchini wakitembelea hifadhi za Taifa na vivutio vingine.
Miongoni mwa watu maarufu waliotembelea vivutio hivyo ni pamoja na mwanamuziki wa Marekani, Usher Raymond na mcheza soka maarufu David Beckham aliyewahi kuchezea timu ya Taifa ya England na timu za Manchester United na Real Madrid.
Mara baada ya kutembelea vivutio hivyo, Usher aliweka picha za ‘matanuzi’ aliyopata akiwa Tanzania, katika mitandao yake ya kijamii ya Twitter na Instagram.
Usher alikuwa ameongozana na familia yake wakiwamo watoto wake wawili wa kiume katika Hifadhi ya Serengeti.
“Safari hii imekuwa ya maajabu, tumefurahi sana kuona uzuri wa mbuga hii nikiwa na familia yangu,” ameandika katika ukurasa wake wa Twitter.
Si hao tu, watu wengine maarufu waliofika ni mcheza filamu wa Marekani, Will Smith na familia yake na mchezaji wa zamani wa timu ya Liverpool, Mamadou Sakho.
Pia, mchezaji wa Everton Morgan Schneiderlin alitembelea vivutio hivyo hivi karibuni akiwa fungate.
Wiki hii, msanii maarufu wa filamu za Bolywood, India, Sanjay Dutt naye aliwasili kwa ajili ya kutembelea vivutio hivyo.
Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limesema kazi kubwa inayofanywa na shirika hilo kutangaza vivutio vya utalii duniani ndiyo iliyozaa matunda hayo.
Msemaji wa Tanapa, Paschal Shelutete alisema lengo lao ni kufikia watalii milioni tatu ifikapo mwaka 2020. Alisisitiza kwamba Tanapa inatathmini namna ya kuwatumia watu mashuhuri wanaotembelea nchini kujitangaza zaidi kimataifa ili kufikia lengo hilo.
Alipoulizwa namna wanavyoitumia fursa ya watu hao mashuhuri kutembelea nchi, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Phillip Chitaunga alisema, “Hili ni jambo ambalo kwetu tunalichukulia kwa mapana yake kwa sasa.”
Akizungumzia vivutio vilivyopo nchini, mwandishi wa habari za usafiri na utalii wa Marekani, Tim Bewer alisema, “Tanzania ina Mbuga nyingi nzuri kama Serengeti na Ngorongoro, wanyama watano bora, simba wapandao miti, kikubwa ni ubora wa hifadhi hizo ambazo zimetumia robo tatu ya ardhi yake kuhifadhi wanyamapori.”
Pia, mtaalamu wa masuala ya safari na utalii na raia wa Uingereza, Phillip Biggs amekaririwa na jarida mtandao la Huffpost akisema, “Hakuna majadiliano, hakuna nchi ya Afrika, kusema ukweli, yenye wanyama wakubwa katika eneo kubwa kama Tanzania.”
Post A Comment: