WASHINDI wa Kombe la FA, Simba wamefanya usajili wa nyota wawili kwa mpigo leo Jumatano kwa kuwasainisha kipa namba mbili wa Taifa Stars, Said Mohammed 'Nduda' na beki, Erasto Nyoni.
Usajili huo wa Simba umekuja katika hali isiyotarajiwa kutokana na awali timu hiyo kuonekana kama imejiimarisha vilivyo, lakini leo uongozi wa timu hiyo umethibitisha kuwasanisha wachezaji hao kwa mikataba ya miaka miwili kila mmoja.
Nduda aliyesaini akitokea Mtibwa Sugar, amesajiliwa maalum kwa kumpa changamoto Aishi Manula ambaye pia amejiunga na timu hiyo akitokea Azam FC.
Katika michuano ya Cosafa iliyoisha hivi karibuni na Taifa Stars kushika nafasi ya tatu, Nduda aliibuka kipa bora wa michuano hiyo ingawa alidaka mchezo mmoja tu wa kuwania mshindi wa tatu.
Kwa upande wa Nyoni aliyesaini akitokea Azam, amesajiliwa mahususi kuziba pengo la Abdi Banda aliyejiunga na Baroka FC ya Afrika Kusini.
Kumbuka kuwa Erasto Nyoni alikuwa mbioni kujiunga na klabu ya Yanga ,hali iliyoelezwa kuwa baadhi ya vigogo wa klabu hiyo walikuwa katika hatua za mwisho kutaka kumsainisha mkataba.
Post A Comment: