NI kioja! Serikali imeduwazwa na kitendo cha kampuni ya Startimes kutoilipa gawio, hivyo kutoa siku saba ikitaka maelezo ni kwa nini imeshindwa kutengeneza faida tangu walipoingia nayo ubia mwaka 2010.
Aidha, serikali imeunda kamati ya wataalamu 10 wa mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ili kutoa taarifa ndani ya muda huo.
Waziri wa wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, ndiye aliyetangaza hatua hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za kuchukuliwa kutokana na ziara ya Rais John Magufuli, aliyoifanya Mei 16, mwaka huu.
Dk. Mwakyembe alitoa taarifa hiyo baada ya kikao cha zaidi ya saa tatu kilichofanyika baina yake na Mwenyekiti wa Startimes, Xinxing Pang, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk. Ayoub Rioba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Dk. Mwakyembe alisema mkataba ulioingiwa na kampuni hiyo haujainufaisha serikali na una changamoto kubwa licha ya kampuni hiyo kufanya kazi kama hiyo katika nchi 32 barani Afrika na kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameshafanya uchunguzi wake.
Alieleza kuwa pamoja na Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuhama katika mfumo wa analogia kwenda digitali, bado ubia huo haujaweza kutoa faida na kuinufaisha serikali.
“Rais alipokuja kufanya ziara katika Shirika la Utangazaji TBC na kisha kutembelea Startimes, alihoji iwapo kuna faida ya kuendelea na huduma za kampuni hii kwa kuwa hakuna faida yoyote ndani ya miaka saba. Nataka kujua sababu za kushindwa kuipa serikali faida,” alisema Mwakyembe.
Alisema katika kikao hicho, Startimes waliahidi kutoa ushirikiano na kwamba kabla ya mwisho wa Julai, serikali itatoa uamuzi.
Mwenyekiti wa Startimes, Pang alisema baada ya kupata taarifa kuhusu suala hilo, aliamua kuja nchini kukutana na serikali kabla haijatoa uamuzi wa jambo hilo.
“Tangu mwaka 2010 kampuni hii imekuwa ikifanya kazi Tanzania kwa ushirikiano mkubwa na serikali, lakini sasa tunataka tufahamu kwa nini hakuna faida,” alisema Pang.
“Kampuni hii iliasisiwa mwaka 2009 kwa ushirikiano na TBC na rais alipouliza maswali kadhaa kuhusu kampuni yetu, tumezingatia maswali hayo na tumejitahidi kujibu… madhumuni yangu ni kujadiliana na Waziri ili tutoe maelezo kuhusu kile tulichokifanya hadi sasa,” alisema.
Post A Comment: