ads

KESI ya madai dhidi ya Mchungaji Josephat Mwingira imechukua sura mpya baada ya mlalamikaji Dk. William Morris kuwasilisha maombi ya kutaka mahakama itoe amri ya kufanyika kwa kipimo cha utambuzi wa vinasaba (DNA) kwa mdaiwa na mke wa mdai ili kubaini wazazi halisi wa mtoto aliyezaa mkewe huyo.


Mlalamikaji Dk. Morris ambaye ni mume wa Dk. Phillis Nyimbi (mlalamikiwa wa pili) anayedaiwa kuzini na mchungaji Mwingira na hatimaye kuzaa naye mtoto, aliwasilisha maombi hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa mlalamikaji, Respicius Ishengoma alidai kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa jana kuwa mahakama hiyo ianze kusikiliza maombi hayo yaliyoungwa mkono na hati ya kiapo, kabla ya kuingia kwenye kesi ya msingi.

Mawakili wa Mchungaji Mwingira na Dk. Phillis waliomba kupatiwa muda ili waweze kuwasilisha majibu yao.
Hakimu Simba aliahirisha kesi ya msingi na maombi hayo hadi Agosti 2 kwa ajili ya kutajwa.

Katika hati hiyo ya maombi, Dk. Morris anaiomba mahakama itoe amri kwake yeye, walalamikiwa mchungaji Mwingira na Dk. Phillis pamoja na mtoto waende kupimwa DNA.

Kupitia hati yake ya kiapo, Dk. Morris anadai Novemba 15, 2013 alifungua kesi ya msingi ya madai namba 306 ya mwaka 2013 dhidi ya Mchungaji Mwingira na Dk. Phillis kwa kuzini na kusababisha kuzaliwa mtoto.

Dk. Morris anadai kutokana na maelezo ya utetezi yaliyowasilishwa mahakamani hapo Desemba 27, 2013 na Mchungaji Mwingira kukana kuzini na Dk. Phillis au kuwa na uhusiano na hatimaye kupatikana kwa mtoto huyo, na kwa kuwa mlalamikiwa wa pili alikubali kuwa na uhusiano na mwanaume wakapime DNA.

"Kwa sababu anazozijua mlalamikiwa wa pili (Phillis), mtoto huyo alimwandikisha kama mie ndiye baba yake mzazi, kitu ambacho siyo cha kweli. Kipimo cha DNA kina nguvu kwa ajili ya kupata utambuzi na kueleza familia ya mtoto huyo,” alidai kupitia hati yake hiyo ya maombi.

Kutokana na hilo, mlalamikaji huyo anaomba mahakama itoe amri ya kwenda kufanywa kipimo hicho ili kuweza kufikia mwisho wa haki.

Katika kesi ya msingi, Dk. Morris pamoja na mambo mengine anaiomba mahakama hiyo imwamuru Mchungaji Mwingira amlipe Sh. bilioni 7.5 kama fidia ya kuzini na kuwa na uhusiano na mkewe Dk. Phillis.

Pia, Dk. Morris anaiomba mahakama itoe amri ya kwenda kupimwa ukimwi wote watatu (mlalamikaji, Mchungaji Mwingira na Dk. Phillis) na kwamba ifanyike DNA kati ya walalamikiwa hao wawili na mtoto.

Kupitia hati yake ya madai, Dk. Morris anadai Mwingira na Phillis waliingia katika uhusiano muda usiojulikana bila kujali kuwa Phillis alikuwa mke wa mtu (mlalamikaji) na baada ya kufanya uchunguzi juu ya uhusiano huo mkewe alidai alibakwa na Mchungaji Mwingira.

“Kubakwa huko kulisababisha sio tu Dk. Phillis kupata ujauzito pia kulisababisha matatizo mbalimbali ya kiafya,” alidai.

Inadaiwa Desemba 28, 2011, mlalamikaji Dk. Morris na Phillis walifunga ndoa katika Kanisa la Anglican, Upanga na wakati wa uhusiano wao (Mchungaji Mwingira na Phillis) waliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na kubahatika kupata mtoto mwenye miaka tisa na matatizo mbalimbali ya kiafya kwa mkewe.

Mlalamikaji huyo anadai alitoa taarifa polisi katika kituo cha Kibaha, ambapo aliambiwa ni suala la uzinzi au udhalilishaji ambalo haliwezi kuwa la kijinai na kushauriwa afungue kesi ya madai.

Dk. Morris anadai kitendo cha mkewe kuwa na uhusiano na Mwingira, ni kwenda kinyume na ndoa yao halali na kimeharibu mipango yake ya mbele kiasi cha kumfanya apoteze matumaini ya kuishi.

“Uhusiano huo umeniaibisha na kushusha hadhi yangu si tu Tanzania na duniani, hivyo kunisababishia niteseke kiakili na kiuchumi,” anadai Dk. Morris.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: