ANAJULIKANA kama mwizi wa kimataifa wa vito vya thamani, akiwa amewahi kusakwa katika mabara matatu ya Ulaya, Amerika na Asia.
Licha ya sasa kuwa na mri mkubwa wa miaka 86 bado hajaachana na wizi, kazi aliyojivunia, ambayo ameifanya kwa miongo sita.
Naam, anajivunia kazi hiyo, kiasi kwamba tangu akamatwe mara ya kwanza, anapoulizwa au anapotakiwa kujaza maelezo kuhusu kazi yake huandika; ‘mwizi wa vito’.
Doris ‘Diamond’ Payne, anahesabiwa kuwa ndiye mwizi mahiri zaidi wa vito duniani na kutokana.
Hupendelea zaidi kuiba vito vya almasi na kwa sababu hiyo jina lake la katikati amebatizwa kama Diamond.
Pamoja na kuwa hakumbuki jumla ya kiasi cha vito alivyoiba tangu aanze shughuli hizo katika miaka ya 1950, inakadiriwa kuwa na thamani ya dola zaidi ya milioni mbili sawa na Sh bilioni nne.
Wakati akiiba hutumia mbinu za kupumbaza kuwafanya wahusika katika sehemu anakoiba wasitambue au wasahau kuwa amebeba vito.
Amekuwa akishitakiwa tangu miaka ya 1950 na simulizi zake zimetengenezewa filamu ya maisha yake; Maisha na Uhalifu wa Doris Payne.
Aidha, muigizaji maarufu mwenye asili ya Kiafrika, Helle Berry amemuigiza mwivi huyo katika filamu mpya kama mwizi mahiri wa kimataifa wa vito.
Mara kadhaa ikiwamo 2013, alidai ataachana na maisha hayo, lakini mazoea yana taabu!
Katika matembezi yake mwaka juzi katika duka lililopo Mtaa wa Saks Fifth, huko Buckhead, Atlanta, ajuza huyo hakuweza kujizuia tabia yake hiyo.
Hata hivyo, bahati mbaya mno kwake, mamlaka tayari zimeshamjua vilivyo kutokana na historia yake na amefungwa kifaa mguuni cha kufuatilia nyendo zake na hivyo kuwa rahisi kumkamata.
Mlinzi aliyekuwa akiangalia video ya usalama alimuona Payne akiingia dukani, alimshuhudia akiingiza mfukoni hereni zenye themani ya dola 690, kwa mujibu wa polisi.
Katika kisa kingine cha karibuni, Doris Payne alikutwa katika duka moja katika eneo la Chamblee mjini Georgia akiwa ameiba vito vyenye thamani ya dola 86. Lakini aliachiwa kwa dhamana kutokana na umri wake.
Katika kesi ya mwaka huu, mfanyakazi mmoja wa duka alisema Doris aliiba vitu kadhaa kutoka kwenye duka la dawa, vifaa vya kielektroniki na katika duka la mboga.
Wakili wake, Drew Finding alinukuliwa na chombo kimoja cha habari akisema: Hiki ni kisa cha kipekee ikilinganishwa na visa vingine vilivyopita.
Tunazungumzia kile bibi wa miaka 86 anachotaka ili kuweza kuishi kila siku, ikiwamo chakula na matibabu.
Akiwa amezaliwa na baba mfanyakazi wa mgodi wa makaa ya mawe na mama mshona nguo katika eneo la kijijini la mji masikini wa Slab Fork, West Virginia nchini Marekani mwaka 1930, Doris Marie Payne alikuwa mtoto wa mwisho kati ya sita wa familia hiyo.
Ijapokuwa familia ilihamia Cleveland, Ohio, alikuwa bado akikabiliana na kukosekana na haki, ubaguzi na ukandamizaji, ambao uliwakabili wanawake wengi weusi nyakati hizo za historia ya Marekani.
Ndoto yake ilikuwa kuwa mwanasarakasi katika moja ya makundi ya muziki, lakini hakuweza kufanikisha kutokana na ubaguzi wa rangi.
Akabaini ili aweze kuishi lazima atafute namna nyingine na hivyo akaondoka katika mji huo mdogo na kwenda kuizuru dunia. Wizi wa vito ukawa kazi yake kuu baada ya kukosa njia mbadala!
Kwa mara ya kwanza alijifunza mbinu za wizi akiwa bado mdogo wakati karani wa duka moja la vito alipomtoa nje kwa nguvu wakati mteja mweupe alipoinga.
Kwa hasira alizokuwa nazo, hakurudi nyuma na akiwa na umri wa miaka 23 tu alitoka katika duka la vito la mjini Pittsburg akiwa na almasi yenye thamani ya dola 22,000 sawa na Sh milioni 44, ambazo ni nyingi mno kipindi kile.
Kutoka hapo akatembelea maduka ghali zaidi duniani akilenga zaidi miji ,ikubwa ya Uingereza, Ufaransa, Italia, kisiwa cha Monaco na hata Japan, ambako huiba na kuuza vito.
Moja zake ni uvaaji mzuri na ghali wa mavazi, begi la mkononi la bei mbaya, tabasamu la kichawi na uwezo mzuri wa kuzungumza kiasi cha kuwapumbaza wafanyakazi wa maduka ya vito.
Kwa mfano ataagiza vito fulani, wakidhani wamepata mteja wa maana, wauzaji watamchangamkia. Yeye atawaambia’ “nileteeni vito vya thamani zaidi hapa.” Hilo linakuwa kosa!
Kwani wauzaji wanapoenda kuleta vito vingine, tayari anapotelea zake na vito vya awali kama upepo wa kisulisuli.
Wakati wa kilele cha umahiri wake wa wizi alihusishwa na majina zaidi ya 20, tarehe nane tofauti za kuzaliwa.
Lakni staili yake ya maisha ilimgharimu huku data zake zikiwa mikononi mwa polisi wa kimataifa. Kuanzia miaka ya 1970 akaanza kujikuta akiingia na kutoka jela na mahakamani.
Mwaka 2010 pia anakumbukwa alipoomba kifungio cha chepesi, akidai anasikitika kwa aliyofanya,’ lakini haikutosha!.
‘Hutaacha wewe,’ Jaji Frank Brown alimkoromea wakati huo, akieleza kwanini ameamua kumpa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela.
Baada ya adhabu hiyo, Doris aliapa kuacha maisha yake ya uhalifu.
Lakini mwaka 2013, miezi mitatu tu baada ya kuachiwa kutoka jela, alirudia akitumia mbinu zile zile za zamani.
Wakati Doris alipoingia katika duka la vito la El Paseo huko Palm Desert, California, wafanyakazi walimkaribisha kwa bashasha.
Kibibi mwenye nywele nyeupee, anayevutia, afya dhoofu lakini akijitutumua alijitokeza.
Aliwaambia alikuwa na malipo ya bima ya dola 25,000 tu na alitaka kutumia fedha taslimu kujinunulia vito.
Wauzaji walimzunguka wakamsaidia kumvalisha cheni na pete alizochagua. Baada ya vito kumkaa vyema aliruka ruka kwa furaha na kucheza kisha akapumzika kitini.
Baada ya kumaliza mpangilio wa namna ya kulipia almasi na pete ya dhahabu kwa siku inayofuata, walimsindikiza hadi mlangoni.
Kile ambacho hawakufahamu wakati huo ni kuwa pete yenye thamani ya dola 22,500 sawa na Sh milioni 45 ilikuwa bado kidoleni mwake.
Meneja wa duka hilo, alibaini kukosekana kwa pete hiyo, saa chache baada ya bibi huyo mwizi mahiri kutoweka.
Mtaalamu huyu mkongwe wa wizi katika kuonesha ameanza kuzeeka, aliuuza pete hiyo kwa dola 800 tu sawa na Sh milioni 1.6 tu tena katika duka la karibu.
Lakini kwa vile alishtukiwa, kama sehemu ya mauzo alitakiwa kusaini dole gumba, ambalo lilisaidia kumkamata.
Hata hivyo kutokana na uzee na afya dhoofu alipewa kifungo kifupi.
Wachambuzi wa mambo ya uhalifu wanasema kwamba ni nadra kwa mhalifu kuendelea na kazi hiyo kwa miaka minvi kiasi hicho, wengi huacha pale wanapopata fedha za kutosha kuanzisha miradi na hawako tayari kuhatarisha tena maisha au kuuawa.’
Post A Comment: