Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Alhaji Kirunda Kivejinja leo, Julai 25 atazungumza na waandishi wa habari kuhusu Bunge la Afrika Mashariki (Eala).
Taarifa iliyotolewa jana Julai 24 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha EAC, Richard Owora imesema Kivejinja ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa Pili na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika wa Uganda, atatoa taarifa rasmi ya kuchelewa kuanza kwa Bunge la Nne la Eala.
"Waziri Kivejinja atawajulisha hatima ya Bunge la Nne la Eala ambalo lilitakiwa liwe limeshaanza majukumu yake lakini hadi muda huu bado kutokana na sababu mbalimbali ambazo atazieleza," amesema.
Pamoja na mambo mengine, majukumu ya Eala ni kupitisha bajeti ya EAC, kufanya kazi ya kusimamia utekelezaji wa mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo na utekelezaji wa mkakati wa maendeleo ya EAC Pia, linatunga sheria za EAC, kufanya kazi za usimamizi wa mihimili mingine na kuwakilisha wananchi wa eneo la jumuiya katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi sita wanachama.
Bunge la Eala lilikuwa lizinduliwe Juni 4 lakini hilo halikufanyika kutokana na Kenya kushindwa kuchagua wabunge wake saba kutokana na sababu ikiwa ni kuingia kwenye kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Post A Comment: