WAZIRI wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amefunguka na kusema alitolewa mbuzi wa kafara katika kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow.
Amesema wabaya wake walijikita kuhoji matumizi ya Sh milioni 10, badala ya Sh bilioni 1.6 alizopokea.
Profesa Tibaijuka ameyasema hayo ikiwa ni miaka miwili na nusu tangu avuliwe uwaziri kwa sababu ya kashfa hiyo.
Katika kashfa hiyo, Profesa Tibaijuka ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kusini, ni mmoja wa watu waliopata mgao wa fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira.
Rugemalira alikuwa mbia wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.
Akizungumza na gazeti hili Dodoma jana, alisema baadhi ya mambo kuhusu suala hilo kama atayaweka wazi yanaweza kuingilia kitabu anachotaka kuandika.
Alisema wakati wabaya wake wakimsakama kwa kauli yake aliyosema kuna Sh milioni 10 alitoa kwenye akaunti yake akisema zilikuwa ni za mboga, vita hiyo ilimsaidia kumuinua badala ya kumuangusha kama walivyotarajia.
“Hili ni swali zuri na kweli sijawahi kufafanua maana yangu ilikuwa nini kusema Sh milioni 10 ni hela ya mboga. Niliona kwamba nilishatolewa mbuzi wa kafara kwa hiyo niachie Mungu.
“Kama akipenda na kunivusha nitapata nafasi ya kueleza jinsi nilivyokumbwa na kadhia hiyo .
“Kumbuka hivi sasa watu wanatumbuliwa kila siku lakini mimi nadhani naingia katika historia ya Tanzania kama mtu pekee aliyetumbuliwa katika Serikali ya Awamu ya Nne, wengine walijiuzulu,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema pamoja na hali hiyo kwa sasa wana CCM katika jimbo lake hawataki ujinga kwa sababu waliweza kumsimamia na kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kura nyingi.
“Bahati nzuri pia tukampata Rais mkweli ambaye naye hataki ujinga na utani usio na maana kuingoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Credit - Mtanzania
Post A Comment: