WAZIRI Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye amesema kuna umuhimu wa kuendeleza mchakato wa Katiba mpya ili kuondoa utata unaoibuka katika mambo ya msingi likiwamo la kuwa na tume huru ya uchaguzi.
Madai ya kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba mpya yamekuwa yakisikika kwa nguvu kwa miezi 16 iliyopita, hata hivyo.
Akihutubia Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chadema (Chaso) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali yao, Sumaye alisema Katiba mpya imewekwa pembeni kwa kuwa watawala hawataki madaraka yao yadhibitiwe.
Sumaye ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu Taifa ya Chadema, alisema Katiba ya wananchi ambayo Tume ya Jaji Joseph Warioba ilipita nchi nzima na kupitishwa na Bunge la Katiba, leo inaonekana siyo jambo la kipaumbele na halionekani itashughulikiwa tena kwa kuwa itawadhiti watawala.
"Mchakato huo wa Katiba mpya umeigharimu nchi fedha nyingi za walipakodi na kuitupa... ni makinikia nyingine," alisema.
"Sisi hatutawashtaki mahakamani, lakini tutawashtaki kwa wananchi. Tunadai Katiba mpya ya wananchi kwa nguvu zote kwa niaba ya wananchi," alisema zaidi Sumaye, mwanasiasa pekee kushika wadhifa wa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo; katika serikali ya awamu ya tatu.
Sumaye alisema mfumo wa vyama vingi vya siasa unaruhusu haki, usawa na uwazi wakati wa kampeni za uchaguzi, upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo, hatua ambayo alidai inaweza kufikiwa kama kutakuwa na tume huru ya uchaguzi.
"Hatuwezi kuwa na tume huru ya uchaguzi wakati wasimamizi wake siyo tu ni watumishi wa serikali bali ni makada wa chama tawala," alisema.
"Unapataje tume huru wakati Rais anawateua baadhi ya makada wa chama chake kuwa wakurugenzi wa halmashauri zetu na hao ndiyo watakaokuwa wasimamizi wa uchaguzi katika kila jimbo la uchaguzi?"
Sumaye alisema vitendo vya ukiukwaji wa haki na vitisho mbalimbali vimekuwa vya kawaida wakati wa kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo na kwamba wakati mwingine aliyeshindwa kwa kura hutangazwa kwa mabavu kuwa ndiye mshindi.
Kada huyo wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema hakuna demokrasia ya vyama vingi vya siasa ya kweli kama hakuna tume huru ya uchaguzi na kwamba mfumo wa demokrasia ya vyama vingi huleta ushindani wa haki wa kisiasa baina ya vyama vya siasa.
Alisema mfumo huo pia huondoa hofu kwa wananchi kuchagua chama wakipendacho na hata viongozi wawapendao bila hila, ghiliba, vitisho wala njama za aina zozote.
"Mfumo huu utaleta maendeleo endelevu kwa ajili ya wananchi kwa sababu ya ushindani wa kisiasa. Demokrasia ya kweli ina tabia ya kujenga vyama viwili vyenye nguvu ambavyo huwa na tabia ya kuwekwa madarakani kila baada ya muda fulani," alisema.
Aliongeza kuwa chama kimoja kikitawala muda mrefu huwa hakina jipya la kuwaletea wananchi kwa sababu hakina kipya cha kufanya madarakani zaidi ya kutafuta matukio ili kuonekana kina jipya kwa wananchi.
Kuhusu nafasi ya Chadema kisiasa, alisema ni vyema wanachama wakatambua nyakati na kutokatishwa tamaa na vitendo vyovyote vya kuwarudisha nyuma na badala yake kuendelea kuwa jasiri kuwapigania wananchi wanyonge.
Post A Comment: