AGIZO la kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinachukua dawa za viuadudu zinazozalishwa katika kiwanda cha dawa hizo kilichopo Kibaha, mkoani Pwani limeanza kutekelezwa kwa Halmashauri 14.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto –Idara Kuu ya Afya, Catherine Sungura, dawa hizo zitaanza kugaiwa katika Halmashauri za mikoa 14 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria.
“Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu anapenda kuwatangazia Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuwa viuadudu vitaanza kugaiwa leo (jana) kwa Halmashauri za Mikoa 14 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa malaria,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mikoa inayoanza kupata mgawo huo, na kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwenye mabano ni Kagera (41%), Geita (38%), Kigoma (38%), Ruvuma (23%), Tabora (20%) na Mtwara (20%).
Mingine ni Mara (19%), Morogoro (14%), Shinyanga (17%), Lindi (17%), Pwani (15%), Mwanza (15%), Katavi (14%) na Simiyu (13%).
Taarifa hiyo imebainisha kuwa mikoa mingine ambayo haijatajwa itagaiwa viuadudu katika awamu ijayo.
Aidha taarifa hiyo imewakumbusha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kufanya upuliziaji wa viuadudu kwa kuzingatia Miongozo ya Wizara ya Afya ili kuwezesha kupata matokeo tarajiwa ya kutokomeza mbu ili kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini.
“Wizara ya Afya inapenda kumshukuru kwa dhati na kumpongeza Mhe. Rais Dk. Magufuli kwa kuongeza chachu katika Mapambano dhidi ya Malaria Nchini,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo akiwa katika hafla ya uzinduzi wa Barabara ya Bagamoyo–Makofi–Msata wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani Alhamisi iliyopita.
Alitoa siku saba kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zimechukua dawa hizo ambazo amezilipia Sh. bilioni 1.3.
Post A Comment: