ads

Spika wa Bunge, Job Ndugai huwa hana simile anaposhughulikia wapinzani na huonekana kama hajali iwapo watamfanyia kitendo chochote, lakini lakini kitendo cha wabunge hao kutohudhuria futari aliyoandaa kimeonekana kumnyima raha.


Kiongozi huyo wa Bunge aliandaa futari kwa ajili ya wabunge wote Jumanne iliyopita, lakini hakupata wote, hasa wa upinzani ambao vyama vyao vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi.

Kutokana na kususa huko kwa wapinzani, Spika Ndugai aliwasihi na kukumbusha umuhimu wa jamii kukaa pamoja, kujadiliana na kumaliza tofauti zao. Alisema, licha ya jukumu zito la kupitisha bajeti na Sheria ya Fedha ya mwaka 2017, ushirikiano wa kijamii ni muhimu.

Awali, jioni ya Jumatatu ya wiki hii, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliandaa futari iliyohudhuriwa na wabunge, wafanyakazi, mabalozi na wageni wengine waalikwa waliokuwapo bungeni siku hiyo na mahudhurio yalikuwa ya itikadi na dini bila ya kujali nyadhifa.

Siku iliyofuata, hali ilikuwa tofauti baada ya Ndugai kufuata nyayo za Majaliwa. Wabunge wa upinzani walisusia, jambo ambalo linaonekana kumkera na kumfanya alizungumzie suala hilo kwa hekima japo hakusahau kutia ‘chumvi’ kidogo.

“Tulihudhuria futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu. Leo nami nimepata nafasi, nimeandaa kama nilivyowataarifuni,” alisema Ndugai.

“Lakini nikajifunza kitu kimoja ambacho sikupenda kukisema ila nikiseme hapa kidogo. Kuna wenzetu wamekatazana rasmi kuhudhuria shughuli kama hizi.”

Ndugai alieleza hayo Jumanne asubuhi wakati akihitimisha kipindi cha maswali na majibu kabla ya kupisha mapumziko mafupi kisha bajeti ya Serikali kupigiwa kura.

Aliwashauri wabunge wenzake kufanya uamuzi kwa busara kwa mujibu wa Katiba ili kuipigia kura bajeti hiyo na kuwakumbusha umuhimu wa kufanya hivyo ili kuiruhusu Serikali kukusanya na kutumia Sh31.7 trilioni zilizopendekezwa kwa mwaka ujao wa fedha.

“Wale wanaotaka kutoka, ruksa. Japo sitarajii lakini ikitokea sitashangaa,” alisema Ndugai.

Taarifa ya kususiwa

Pamoja na masuala ya bajeti, Spika Ndugai alionekana kuwa na taarifa za wanaotaka kususia futari.

Alisema Bunge linaendeshwa kwa mawasiliano ya namna mbalimbali baina ya wabunge na uongozi, hivyo endapo kuna jambo linakwaza na kusababisha watu wasipate futari pamoja ni vizuri viongozi wakae na kuondoa vikwazo hivyo.

“Kama havipo, basi ushauri wangu tuwe tunajumuika kwa sababu sera hizo zikienea matokeo yake ni mpasuko ambao hakuna anayeuhitaji hapa,” alitahadharisha.

Pamoja na tahadhari hiyo, alisema hataki kuingilia uhuru wao kwa kuwa wana haki ya kufanya hivyo kama wanaona ni sawasawa.

Hata hivyo, aliwashauri viongozi waliotoa agizo hilo kwamba jambo hilo ni la kijamii linalohitaji ushiriki wa waliopo na ikifika mahali kiongozi anawazuia watu kwenye mambo ya kijamii, ajue anaenda mbali.

Ndugai alisema kinachofanywa si busara hasa kwa mwezi huu mtukufu wa kusamehe hata maadui na kutoa mkono upande wa pili katika kukamilisha ibada iliyokusudiwa. “Siyo mwezi wa chuki na kubaguana. Niwakaribishe tena kwenye futari kwa watakaoweza kufika. Watakaoshindwa inshallah kila la heri. Tutaendelea kuwa pamoja mjengo huuhuu,” alisema akihitimisha nasaha zake.

Kura ya hapana

Baada ya kupitishwa kwa bajeti jioni ya siku hiyo, Ndugai aliwataka mawaziri kuwatambua wabunge waliopiga kura ya hapana na kutopeleka fedha za miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao kwa kuwa ndicho walichokataa.

Wabunge kadhaa wa chama tawala waliunga mkono hoja hiyo, lakini ilipingwa kwa nguvu na wapinzani.

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi aliyeomba mwongozo wa Spika, alisema fedha hizo zinatokana na kodi za wananchi na endapo itazingatiwa Serikali isikusanye fedha kwenye majimbo yao.

“Serikali inakusanya kodi kutoka kwa wananchi wote na mapato yake ndiyo yanatumika kutekeleza bajeti,” alisema Mbilinyi.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: