Simba inaendelea na zoezi la usajili lakini hilo halijaifanya klabu hiyo ishindwe kushiriki kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao utafanyika Agosti 12 mkoani Dodoma sambamba na ule wa chama cha soka cha wanawake Tanzania (TWFA) utakaofanyika Julai 8.
Jumla ya wajumbe wanne wa kamati ya utendaji ya Simba, wameamua kujiweka kando na zoezi la usajili na kujikita kwenye chaguzi hizo za taasisi mbili kubwa zinazosimamia mchezo wa soka kwa wanaume na wanawake nchini. Mchujo wa majina ya TFF utatangazwa wikiendi hii.
Awali, wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu', Ally Suru na Said Tully walichukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa TFF.
Kaburu ni Makamu wa Rais wa Simba hivyo anaingia moja kwa moja katika Kamati ya Utendaji.
Kaburu alichukua fomu za kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF wakati Suru akichukua fomu ya kuwania kuiwakilisha mikoa ya Dodoma na Singida kwenye Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo sambamba na Tully ambaye anawania kuwakilisha kanda ya Dar es Salaam.
Wakati vigogo hao wakiwania nafasi hizo kwa upande wa TFF, Mwanamama pekee katika Kamati ya Utendaji ya Simba, Jasmin Badoo naye ameamua kuwaunga mkono kaka zake kwa kujitosa kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama cha soka cha wanawake Tanzania.
Jasmin alisema kwamba; "Nimechukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ya chama cha soka cha wanawake,baada ya kuona nakidhi vigezo ambavyo vinahitajika ili kuleta maendeleo ya soka la akina mama."
Post A Comment: