WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema atazifuta mara moja taasisi zisizo za kiserikali zinazohamasisha kudai haki ya wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni baada ya tamko la Rais John Magufuli linalotaka wasirudi baada ya kujifungua.
Mwigulu alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati wa uzinduzi wa harambee ya ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Bikira Maria, Parokia ya Kisasa ya Kanisa Katoliki.
Mwigulu alisema taasisi yeyote inayohamasisha kudaiwa kwa haki ya wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni pamoja na zinazohamasisha ushoga, usajili wao utafutwa mara moja.
Katika harambee hiyo ambayo alimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mwigulu alisema ingawa Rais Magufuli amekataa wanafunzi watakaopata mimba shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua, katika hali ya kushangaza, suala hilo limekuwa agenda na kuzua mijadala mbalimbali.
Waziri huyo alisema serikali haitaomba ushauri wala maoni kwa yeyote kwa sababu maelezo yaliyotolewa na Rais Magufuli ni maagizo ya serikali.
“Kuna watu wanapenda ‘debate’ (mjadala) hata kwenye masuala ambayo ni maelekezo," alisema waziri Mwigulu. "Tunadhania ni ‘debate’."
"Wengine wanaosema hivi ni waumini na wengine wanaopigia kampeni ni waumini, lakini nyinyi waumini... ni Biblia na vitabu vingine vya dini gani inayosema hayo?”
Mwigulu alisema maandiko aliyopitia yote yanazuia mimba nje ya ndoa na yote yanazuia ndoa za utotoni.
“Nashangaa kuna watu wanataka mimba zihalalishwe kwa wanafunzi wanaosoma!" Alisema.
"Hivi hawa wanasoma kitabu gani cha dini? Na wengine ni kina mama... hayo malezi tunayotaka kuruhusu wanafunzi wafanye mambo hayo msingi wake unatokana na nini?”
Mwigulu alisema anaunga mkono kauli ya Rais kwa asilimia 100 na kuwaomba Watanzania wamuunge mkono Magufuli kwa kuwa serikali imetoa haki ya kila mtoto kupata elimu kwa kuifanya iwe bure kwa hiyo atakayeikosa asitafute kisingizio.
“Serikali haiwezi kuwa na utaratibu huo wa likizo ya uzazi," alisema.
"Kwa mimi ninayesimamia idara ya utekelezaji wa maelekezo, nizionye taasisi zote zilizokuwa zikifanya kazi ya kutetea (sasa) watafute shughuli nyingine za kufanya.
“Rais pale Bagamoyo ameongea mambo makubwa mawili. La kwanza likiwa la mimba na la pili likiwa la ushoga.
"Hili la ushoga linaletwa kwa kivuli cha haki na hili la mimba (nalo) linataka liletwe kwa kivuli cha haki.”
Alisema kwa kuwa wizara yake ndiyo inayosajili taasisi hizo, zitafutiwa usajili wao na kama ni raia wa Tanzania anaendesha kampeni hiyo atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Post A Comment: