Mbunge wa Mkuranga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdallah Ulega amewafananisha wabunge wa upinzani na popo kuwa hawaeleweki na kusema wamekuwa watetezi wa wawekezaji ambao wao wamewatuhumu kuwa ni wezi wa madini.
Mbunge huyo amesema hayo bungeni akisema kuwa wapinzani hao leo limewashuka baada ya jana Rais Magufuli kukutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton na kukubaliana kuwa kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.
"Popo hajafahamika kama ni mnyama au ndege mpaka hivi leo na hawa wenzetu hata sitaki kuwaita vinyonga naomba niwaite popo maanake hawajafahamika kama ndege au wanyama na leo limewashuka kwani walijigeuza kuwa mawakili wa wale ambao sisi tunawatuhumu kwamba ni wezi wetu na yule anayehusika Mkuu amewathibitishia mchana wa leo (jana) ameingia na amekiri mwenyewe kwa kinywa chake ya kwamba wapo tayari kulipa pesa ambazo tunawadai na tena lile lililokuwa linaonekana jambo gumu la kujenga kinu cha kuchenjua madini amelichukua na amesema yupo tayari kujenga" alisema Ulega
Mbunge huyo alikwenda mbali zaidi na kesema bara la Afrika limekuwa na bahati mbaya kwani wapinzani wa Afrika wamekuwa wakitumika na mabeberu miaka yote na kusema wao kama Chama Cha Mapinduzi wanakila sababu ya kutamba kwa kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeweka sawa na kutamka namna nzuri ya kusimamia shughuli za madini.
Post A Comment: