Kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njetwe maarufu ‘Scorpion’ imekwama kuendelea kusikilizwa kwa mara ya tano mfululizo baada ya Hakimu alinayesikiliza shauri hilo kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo iliyopo Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeshindwa kuendelea leo Alhamisi baada ya Hakimu Mkazi, Flora Haule anayesikiliza shauri hilo kuwa mgonjwa na kushindwa kufika mahakamani.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ritha Tarimo aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 20, mwaka huu.
Mpaka sasa mashahidi wanane wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya mshtakiwa Scorpion anayekabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wakili wa Serikali, Chesensia Gavyole alidai mahakama hapo kuwa upande wa mashtaka tayari ulikuwa na shahidi ambaye alipaswa kuendelea kutoa ushahidi leo.
Itakumbukwa kuwa April 18, mwaka huu, kesi hiyo ilishindwa kuendelea baada ya shahidi kuwa mgonjwa na kushindwa kufika mahakamani.
Mei 2, mwaka huu kesi hiyo iliahirishwa baada shahidi namba nane, ambaye alitakiwa kuulizwa maswali na wakili wa utetezi, kuwa mgonjwa kwa mara ya pili.
Pia, Mei 15, mwaka huu, kesi hiyo ilishindwa kuendelea baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na shahidi na Mei 25 kesi hiyo iliahirishwa kutokana na wakili wa utetezi, Juma Nassoro kushindwa kufika mahakamani.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Scorpion alitenda kosa hilo Septemba 6, 2016 Buguruni Sheli wilayani Ilala, ambapo alimjeruhi Said Mrisho.
Katika shtaka la kwanza, Scorpion anadaiwa kuiba cheni moja ya shingoni aina ya silva yenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh60,000, bangili moja ya kiume yenye thamani ya Sh85,000 , pochi na fedha taslimu Sh331,000 na kwamba thamani ya vitu vyote ni Sh476,000 mali ya Mrisho.
Katika shtaka la pili, mshtakiwa alimjeruhi kwa kumchoma kisu Mrisho sehemu ya machoni, mabegani na tumboni ili aweze kujipatia mali hizo bila kikwazo.
Post A Comment: