Kodi mpya ya asilimia moja iliyoongezwa katika madini yatakayokuwa yanasafirishwa nje, itaipatia Tanzania zaidi ya nusu ya mapato ambayo nchi ilikuwa inapata katika mirabaha inayolipwa na kampuni za uchimbaji.
Kodi hiyo imo kwenye mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yaliyosomwa juzi bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18.
Hadi sasa, kampuni hizo zinalipa mirabaha ya hadi asilimia 4 ya madini yanayouzwa nje, lakini mabadiliko hayo yatazikamua zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) ya mwaka 2016, mauzo ya dhahabu nje yalikuwa dola 1.8 bilioni za Kimarekani (sawa na Sh3.96 trilioni)
Kwa maana hiyo, iwapo kodi hiyo ingetozwa kwa mwaka huo, Serikali ingepata ziada ya Sh39.6 bilioni kwa mwaka huo.
Pia mauzo ya almasi nje yalikuwa dola 82.18 milioni za Kimarekani (sawa na Sh180.79 bilioni) na kama Serikali ingekata asilimia moja ya fedha hizo, ingepata Sh1.807 bilioni, huku wachimbaji wadogo waliouza dhahabu ya Sh106.7 bilioni, wangeipa Serikali Sh5.3 bilioni za ziada kwa kuongezewa kodi hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, Serikali ingelipwa jumla ya Sh46.707 bilioni za kodi hiyo mpya kwa mauzo ya madini yote kwa mwaka 2016.
Kiwango hicho ni zaidi ya nusu ya mapato yote ya mrabaha ambao Serikali hupata kwa mwaka. Serikali ililipwa mrabaha wa Sh76.1 bilioni.
Kumekuwepo na mjadala wa muda mrefu kuhusu mikataba ya madini, ambayo wengi wanatuhumu kuwa inainyonya nchi.
Mwezi Machi, Rais John Magufuli alisimamisha usafirishaji nje wa mchanga wa dhahabu na shaba na baadaye kuunda kamati mbili za kuchunguza kiwango cha madini kilichokuwa katika makontena yaliyozuiwa bandarini na nyingine kutathmini athari zinazotokana na kusafirisha mchanga huo nje na kuangalia mikataba.
Tayari kamati ya kwanza imeshakabidhi ripoti inayoonyesha kuwa Acacia ilidanganya.
Post A Comment: