Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Onoratus Mwinuka aliyepotea wiki mbili, mwili wake umekutwa umefukiwa kwenye pori la Mlolo Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mke wa Marehemu, Frida Msabi akizungumza na Nipashee juzi kwenye pori hilo ambalo mwili huo ulionekana alisema Machi 14, mwaka huu, mume wake alichukua fedha ambazo alitaka kwenda kununua gari aina ya Pick Up.
Alisema kabla ya kuondoka nyumbani alipopiga hatua chache alimwita mtoto wake Gweni na kumtaka achukue mfuko wa fedha hizo na ufunguo akazihifadhi chumbani kwake(kwa marehemu).
Alisema mume wake alimwambia mtoto kuwa ndani ya chumba hicho kwenye kabati kuna fedha zingine hivyo ahakikishe anafunga chumba hicho.
Alisema wakati akitoa maelekezo hayo ilikuwa ni saa 9:00 usiku muda ambao mume wake amekuwa akiondoka nyumbani kwenda Makumbusho kusambaza maziwa anayouza.
Baada ya kumkabidhi mkoba mtoto alisema aliondoka kwa baiskeli akiwa ameambatana na Ayub.
Mama huyo mfiwa alisema Ayub alidai kuwa walipofika kibao cha Shule ya Sekondari Mabwe Pande usiku huo ghafla ilitokea gari aina ya Noah na kusimama kisha kuwauliza kama wanakwenda.
Baada ya hapo alisema mume wake hakuonekana hadi siku ya nane alipokutwa amefariki dunia na mwili wake ukiwa katika pori hilo.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Suzan Kaganda alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea kwani iliita bila majibu.
Post A Comment: