Mbunge wa Kigoma mjini kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo Mhe. Zitto Kabwe amesema hajakata tamaa na kukataliwa kwa hoja yake binafsi iliyotaka kuundwe tume ya kuchunguza vitendo vya uhalifu hasa utekaji na uteswaji kwa watu wasiokuwa na hatia.
Kupitia mtandao wa kijamii, Zitto amewataka wananchi wawaunge mkono kwenye ajenda ya kuufumua mfumo wa Usalama wa Taifa ili waweze kuunda idara itakayosimamia usalama na maslahi ya taifa badala ya kuteka na kutesa watu.
"Hoja binafsi kuhusu kuundwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza vitendo vya utekaji na uteswaji imekataliwa jana. Hata hivyo, tutaendelea na hoja hiyo wiki ijayo baada ya mapumziko ya Pasaka ambapo waziri mwenye kuhusika na Usalama wa Taifa ataleta hoja ya makadirio ya matumizi ya idara hiyo. Tunataka Idara ya Usalama ifanyiwe marekebisho makubwa ikiwemo kuvunjwa na kuundwa upya. Wananchi tunaomba mtuunge mkono kwenye ajenda hii ya kuufumua mfumo wetu wa usalama wa taifa ili kuunda idara inayosimamia usalama na maslahi ya taifa badala ya Idara ya kuteka na kutesa watu." Ameandika Zitto
Kwa upande mwingine Mbunge huyo amesikitishwa na matukio yanayozidi kutokea katika nchi huku akisema laiti kama kungekuwa na usalama taifa imara pasingekuwa yanatokea vitendo vya utekaji.
Post A Comment: