![ads](http://1.bp.blogspot.com/-J5aEnGVep5k/WJTrf2fzuPI/AAAAAAAAU5U/_iuE-DY1RHAM5_hqPHb-UuNbabG2xn2nwCK4B/s1600/AdvertiseHere.jpg)
Baadhi ya wawekezaji
kutoka China wamesema kupanda kwa gharama za maisha, hali ngumu ya
uchumi na makato makubwa ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
kumewasababishia hasara iliyowafanya baadhi yao kukimbilia nchi za
jirani na wengine kurejea kwao.
Wawekezaji
hao walikuwa wakizungumza wakati wa ziara ya timu ya waandishi wa
habari wa China na Tanzania yenye lengo la kufungua pazia la ushirikiano
wa vyombo vya habari baina ya nchi hizo mbili katika kuandika na
kutangaza taarifa za uwekezaji zinazofanywa na nchi hizo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni ya Sunshine Group, Tonny Sun alisema tozo ya
asilimia 18 ya VAT ni kubwa hasa kipindi hiki ambacho biashara nyingi
zimeyumba.
Sun
alisema ikiwa hali ya biashara itaendelea kama ilivyo, inahatarisha
uwekezaji japo kampuni yake iliyotumia zaidi ya dola 100 milioni (Sh216
bilioni) kuwekeza nchini inaendelea kujitahidi ili ifikie malengo yake
ya kuwasaidia wananchi.
“Hali
ya biashara imekuwa ngumu sana, wenzetu wengine kama asilimia 30 ya
wawekezaji wa China wameshindwa kwa sababu hali ya biashara imekuwa
ngumu, wapo waliohamia nchi za jirani na wengine wamerudi nyumbani, hali
ya biashara imekuwa ngumu,” alisema.
Alisema
kampuni yake yenye viwanda zaidi ya vitano vikiwamo vya kuzalisha
mafuta ya alizeti na korosho, imeajiri wafanyakazi wazalendo 1,600 na
kwamba wakulima wanaowauzia mazao kwa ajili ya kutengeneza bidhaa zao,
wananufaika na uwepo wa soko la uhakika.
Aliiomba Serikali
isaidie kupunguza kodi kwenye baadhi ya bidhaa za msingi zinazochangia
kuinua pato la wananchi wa chini ili kuwawekea mazingira mazuri ya
kuendelea na kazi yao.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Star Times, Leo Liao alisema kwa sasa kampuni yake
haipati faida kutokana na hali ngumu ya uchumi iliyosababisha asilimia
50 ya wateja wake kushindwa kulipia gharama za ving’amuzi kwa mwezi.
Alisema hali hiyo imewafanya wapunguze bei hadi kufikia Sh6,000 kwa mwezi lakini bado hali imekuwa ngumu.
“Hakuna
faida na tunajiendesha kwa hasara kwa sababu ya hali ngumu iliyopo,
ninavyoona tunaelekea kufa kabisa kibiashara kwa sababu asilimia 50 ya
wateja wetu hawajaweza kulipia huduma. Tunajitahidi kuendelea kutoa
huduma nzuri kwa wateja wetu, tumepunguza bei na wateja wanaweza kulipia
kwa siku tano hadi wiki moja,” alisema.
Aliiomba
Serikali kufuta chaneli zinazoonekana bure ikiwa mteja atashindwa
kulipia gharama kwa madai kuwa jambo hilo pia linachangia watu
kutolipia.
“Hali ya uchumi imekuwa ngumu na kwa sababu chaneli nyingine ni bure, basi unakuta watu hawalipii kabisa,” alisema.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: