BAADA ya Rais John Magufuli kulipiga marufuku Jeshi la Magereza na
majeshi mengine nchini kuruhusu askari wake kununua sare kwa watu
binafsi, askari wa jeshi hilo wameibuka na kudai kuwa wamekuwa wanauziwa
sare hizo kwa Sh 45,000.
Pia wamesema kofia na mikanda licha ya kuwa haiuzwi kwenye maduka ya
watu binafsi, lakini upatikanaji wake pia ni wa shida, hali ambayo
inawalazimu askari kutoa rushwa kwa wahifadhi bohari ili kupatiwa sare
hizo.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, askari mbalimbali waliohojiwa licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa kulikemea suala
hilo, walisema ni rahisi kushona kombati uraiani kwa kuwa vitambaa
vinapatikana madukani, lakini kofia na mkanda ikichakaa askari
analazimika kutoa pesa ili kupata mavazi hayo.
“Hizi kofia na mikanda inatolewa bohari ya jeshi, lakini kuupata huko
mkanda au kofia lazima utoe rushwa kwa askari anayefanya kazi pale,”
alisema mmoja wa askari aliyehojiwa na gazeti hili.
Wengi wa askari hao walisema kutokana na ugumu wa kupatikana na kofia
na mikanda ya jeshi hilo, wengi wao wanaendelea kutumia kofia na
mikanda waliyopewa wakati wanamaliza mafunzo.
Walisema kinachotolewa bure na jeshi hilo kwa sasa ni vyeo tu na sio
sare nyingine yoyote. “Kofia hii ninayotumia pamoja na mkanda ni ile
niliyopewa wakati namaliza depo (mafunzo) mwaka 2001,” alisema askari
huyo ambaye ana miaka 15 sasa kazini na kuongeza, “Magereza wanachotoa
bure kwa askari wao ni zile alama za cheo tu, vingine vyote vinavyohusu
sare lazima askari ajinunulie.”
Wakati askari Magereza wanajinunulia sare, serikali imekuwa inatoa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwahudumia askari hao.
Mfano, katika bajeti ya mwaka 2015/16 serikali ilitoa Sh bilioni 167.1 kwa jeshi hilo.
Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 67.7 zilitolewa kwa jeshi hilo kwa
ajili ya matumizi mengineyo, Sh bilioni 97.7 kama mishahara na fedha za
maendeleo zilizotolewa kwa polisi ni Sh bilioni 1.6 Askari mmoja ambaye
yuko mkoani Simiyu aliyefanya mahojiano na gazeti hili, alisema
upatikanaji wa sare za Magereza kwa askari walioko mikoani ni mbaya,
kwani wamekuwa wanalazimika kununua suruali na shati kati ya Sh 40,000
na 45,00 na viatu Sh 40,000.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: