![ads](http://1.bp.blogspot.com/-J5aEnGVep5k/WJTrf2fzuPI/AAAAAAAAU5U/_iuE-DY1RHAM5_hqPHb-UuNbabG2xn2nwCK4B/s1600/AdvertiseHere.jpg)
SERIKALI kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA),
imeokoa Sh bilioni 1.3 baada ya wakala huyo kununua kwa pamoja magari
392 katika mpango wa serikali wa manunuzi ya pamoja.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa GPSA, Jacob Kibona alisema jana kuwa, fedha
hizo zimeokolewa na serikali baada ya kununua magari 392 kwa pamoja kwa
Sh bilioni 56.1 badala ya Sh bilioni 58.1 iwapo kila taasisi ingenunua
magari yake.
“Kwa kweli huu mpango wa manunuzi ya pamoja ni mpango mzuri sana
ambao unaiwezesha serikali kuokoa fedha nyingi,” alisema Kibona na
kuongeza kuwa fedha zilizookolewa zitaiwezesha serikali kufanya shughuli
nyingine za maendeleo ya umma na kama vile kuboresha miundombinu ya
barabara, huduma za afya na elimu.
Aliongeza kuwa, taasisi yake pia katika kipindi cha Julai hadi Oktoba
mwaka huu, imezikabidhi taasisi za serikali magari ya aina mbalimbali
yapatayo 136.
Aidha, alisema katika kuhakikisha wanapunguza gharama katika
manunuzi, wamekuwa wakinunua bidhaa kutoka kwa wazalishaji moja kwa moja
ila inaposhindikana kutokana na sera za kampuni kubwa kuwa na mawakala
wa usambazaji wamekuwa wakinunua kwa mawakala hao kwa makubaliano
maalumu ya kupunguza bei.
Alisema kazi nyingine muhimu ya taasisi yake ni kugomboa mizigo
kupitia bandarini, viwanja vya ndege na mipakani kwa niaba ya serikali
ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita waligomboa mizigo yenye thamani ya Sh
bilioni 62.7 ikiwamo ya Mkongo wa Taifa, vifaa vya Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Aliongeza kuwa kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, pia
walikomboa vifaa mbalimbali vya serikali zikiwamo ndege mbili
zilizonunuliwa na serikali kutoka Canada aina ya Bombardier, vyote
vikiwa na thamani ya Sh bilioni 100.97.
Alisema GPSA ina majukumu mengi, ikiwa ni pamoja kuhifadhi vifaa kwa
ajili ya taasisi za serikali, kutoa huduma ya mafuta kwa magari ya
serikali na kadhalika.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: