MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian
Lubuva ameitaka serikali kubadili muundo wa tume hiyo ili iwe na ofisi
na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar.
Amesema hatua hiyo itawezesha NEC kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi, badala ya kutegemea wakurugenzi wa halmashauri (Ma-DED).
Alisema hayo jana mjini hapa wakati akikabidhi taarifa ya tathimini
baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.
Tathimini hiyo imetolewa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais wa Awamu ya
Tano, Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo.
Lubuva alisema serikali ifanyie mapitio ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi
Sura ya 343 na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 292 ili kurekebisha
vifungu vinavyokinzana.
“Pamoja na hayo, serikali inatakiwa kubadili muundo wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi ili kuwa na ofisi na watumishi katika kila halmashauri
nchini na ofisi ya Zanzibar, hiyo itafanya tume ifanye kazi zake kwa
uhuru zaidi tofauti na sasa kazi hizo zimekuwa zikifanywa na wakurugenzi
wa halmashauri,” alisema.
Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, tume iliamua kufanya
tathimini kwa lengo la kupata mrejesho juu ya utekelezaji wa Uchaguzi
Mkuu kutoka kwa wadau. Alisema ni mara ya kwanza kwa tume kufanya
tathimini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.
“Tathimini hii imefanyika ikiwa ni mojawapo ya zoezi linalokamilisha
mzunguko wa uchaguzi na kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mwingine,”
alisema.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: